KIUNGO wa Singida Black Stars, Morice Chukwu amesema licha ya ushindani kuwa mkubwa, lakini Singida Black Stars ni timu kubwa katika Ligi Kuu Bara, ila makali yake hayaonekani kwa sababu ya Simba na Yanga.
Chukwu ambaye alitua Bongo kwa mara ya kwanza akiwa na kikosi cha Rivers United ya Nigeria katika michuano ya Kombe la Shirikisho, ambayo yalimpa shavu Singida na kusaini mkataba wa miaka mitatu unaomalizika mwishoni mwa msimu huu.
Hapo awali kabla ya kutua Singida gazeti hili liliwahi kuandika, timu zote mbili (Simba, Yanga), ziliwahi kutaka huduma yake, kutokana na kile alichokionyesha kwenye michuano ya kimataifa.
Akizungumza na Mwanaspoti, Chukwu alisema kikosi cha Singida kina ukubwa wake, lakini bado wengi hawauoni kwa sababu ya uchache wa mashabiki.
Alisema miongoni mwa vikosi vyenye wachezaji bora hapa Tanzania huwezi kuiacha Singida, ila Simba na Yanga zinafunika kwa sababu ya mashabiki na umri mkubwa ulionazo katika mshindano haya.
“Singida ina timu kubwa ila sababu ya kwa nini watu wanaiona kama iko chini ni kwa sababu hatuna mashabiki wengi kama ilivyo kwa Simba na Yanga.
“Ila kwa sasa nina furaha kwa sababu ya aina ya kocha ambaye tunae, tunaamini tutakwenda pamoja mbali zaidi ya makadirio ya watu ambayo wameiwekea Singida.”
Aliongeza; “Kwa sasa iwe katika ligi ya ndani au kimataifa tunauwezo wa kujitamba tunaweza kuifunga timu yoyote itakayokuja mbele yetu.
“Siri kubwa ni tumefundishwa kuona mechi zote kama fainali na mtazamo huu umetufanikisha mapema unaona hata kwenye michuano ya Cecafa na huu ni mwanzo tu, yajayo yanafurahisha.”
Singida imebeba Kombe la Cecafa kwa mara ya kwanza Juzi, ikiwa ni fainali zilizopigwa katika uwanja wa KMC na iliilaza Al Hilal mabao 2-1.
Hata hivyo, itakuwa na mechi ya kimataifa, hatua za awali dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda, mchezo utakaochezwa Jumamosi Septemba 20, kuanzia saa 1:00 jioni.