Dar es Salaam. Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), Mhandisi Mkama Bwire amesema upatikanaji wa maji Dar es Salaam na mkoa wa Pwani uko vizuri.
Bwire ametoa kauli hiyo leo Septemba 18, 2025 baada ya kufanya ziara ya kukagua hali ya upatikanaji wa maji katika Wilaya ya Ubungo, maeneo ya Mburahati, Magomeni, na Ilala maeneo Saranga na Kinyerezi.

Ziara hiyo ililenga kujionea hali halisi ya upatikanaji wa maji na kutafuta suluhisho katika maeneo yenye changamoto za huduma hiyo.
“Huduma ya maji katika eneo letu la huduma yaani Dar es Salaam na Pwani iko vizuri na leo tunapita mitaani kukagua na kujiridhisha upatikanaji wa huduma tunayozalisha kama inawafikia wananchi na iwapo kuna changamoto tunazitatua,” amessma Mhandisi Bwire

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Kinyerezi Hassan Nandeta, aliishukuru Dawasa kwa hatua madhubuti ilizochukua katika kuboresha huduma ya maji safi kwenye maeneo yao, akibainisha kuwa wananchi wameanza kunufaika na maboresho hayo.
Dawasa inaendelea kutekeleza mkakati wa kuboresha huduma za maji safi na usafi wa mazingira kwa wakazi wa Dar es Salaam na maeneo jirani, ikiwa ni sehemu ya dhamira yake ya kuhakikisha kila mteja anapata huduma bora na ya uhakika.