Rukwa. Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Charles Makongoro amesema uzinduzi wa dawati maalumu la uwezeshaji biashara ni hatua muhimu itakayowawezesha wafanyabiashara kuendesha shughuli zao kwa weledi na kuchangia ustawi wa Taifa.
Akizungumza leo Alhamisi Septemba 18, 2025, katika viwanja vya ofisi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Rukwa wakati wa uzinduzi wa dawati hilo, Makongoro amesema litawawezesha wafanyabiashara kulipa kodi kwa uelewa mpana zaidi.
Nyerere wakati akizungumza na wafanyabiashara waliojitokeza katika uzinduzi huo
Ameongeza kuwa dawati hilo litarahisisha pia upatikanaji wa taarifa za kikodi kwa wakati sambamba na kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili walipakodi.
“Litumieni vyema dawati hili kwa manufaa ya shughuli zenu za kibiashara, ikiwemo kutatua changamoto zinazowakabili. Dawati hili litawanufaisha,” amesema Makongoro.
Baadhi ya wafanyabiashara wakielezea namna ambavyo watanufaika na dawati hilo
Aidha, amewataka wafanyabiashara wote mkoani humo kulitumia ipasavyo dawati hilo kwa manufaa ya shughuli zao, huku akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kusimama nao bega kwa bega kuhakikisha biashara zinafanyika kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa.
Kwa upande wake, Meneja wa TRA Mkoa wa Rukwa, Husna Nyange amesema dawati hilo litakuwa kiunganishi muhimu kati ya Serikali na wafanyabiashara kwa kutoa taarifa sahihi na za haraka kuhusu masuala ya kodi, pamoja na kusaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza.
Mkuu wa mkoa wa Rukwa wakati akizindua dawati maalumu la uwezeshaji biashara
Baadhi ya wananchi na wafanyabiashara waliohudhuria uzinduzi huo akiwamo Martha Kataila, wameipongeza TRA kwa hatua hiyo. Kataila amesema dawati hilo litaboresha zaidi uhusiano kati ya Serikali na wafanyabiashara na kuwa chachu ya maendeleo ya biashara mkoani Rukwa.
