Dar es Salaam. Wakati wimbi la wafanyabiashara mtandaoni wakiwamo wa vipodozi likizidi kuongezeka, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limesema linaendekea na maboresho ili kuangalia namna gani wanaweza kuzidhibiti ubora wa bidhaa mtandaoni.
Hilo limesemwa wakati ambao mitandaoni kumeibuka wimbi la wafanyabiashara hasa wa vipodozi ambao wamekuwa wakiandaa bidhaa kwa kuchanganya vitu mbalimbali na kuuza kwa wananchi, huku baadhi wakiwaahidi wanunuzi matokeo mazuri ikiwemo kufuta makovu.
Akizungumza katika mkutano wa wahariri na waandishi wa vyombo vya Habari jijini hapa leo Septemba 18, 2025, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk Ashura Katunzi amesema lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha bidhaa zinazokwenda kwa watumiaji zinakuwa salama.
Dk Katunzi amesema dunia inabadilika kutokana na ukuaji wa teknolojia jambo ambalo linafanya kuibuka kwa changamoto nyingine kwani hapo awali haikutarajiwa kama watu watafanya biashara mitandaoni.

Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk Ashura Katunzi, akizungumza katika mkutano wa wahariri na waandishi wa vyombo vya Habari jijini Dar es Salaam.
Amesema kama taasisi wamekuwa wakiziona bidhaa hizo na wanaendelea kuzifanyia kazi na nyingine ambazo zina matangazo wameanza kuyadhibiti kwa kuangalia ni namna gani yaende hewani.
“Tunaendelea na jitihada kuhahakisha bidhaa za vipodozi zinakuwa na ubora na zimesajiliwa kwa ajili ya matumizi ndiyo maana TBS tuna makubaliano ya mashirikiano na Tamisemi (Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa) kwa ajili ya kusaidia katika suala hili kupitia halmashauri zilizopo,” amesema Dk Katunzi.
Amesema kwa kawaida wamezoea kudhibiti kwa kutembelea eneo la kazi lakini sasa wanataka kuhama huko.
“Mmeona wenzetu wa mamlaka ya mapato walitoa mwongozo wa namna ya kulipia kodi za biashara mtandaoni hata kama mtu hana duka lakini anatakiwa kulipia na sisi tunaendelea kuhakikisha bidhaa zina ubora.
“Haimaanishi wanaouza hatuwafuati, tunaziangalia na zile ambazo hazifikii vigezo tunaendelea kuwafuata tunajua wapo bado ni wengi lakini hatua zinaendelea kuchukuliwa,” amesema.
Amesema kwa bidhaa ambazo haziendani na mila na taratibu za Tanzania wameendelea kuzifuatilia na kuhakikisha wanafuata utaratibu.
“Lakini kwa sababu ni mtandaoni, wadau wanaweza wasizijue au kuzifahamu moja kwa moja,” amesema.
Hadi sasa jumla ya bidhaa 8,199 zilisajiliwa na maeneo 47,886 yalisajiliwa sambamba na kuhakiki ubora wa bidhaa na magari yaliyotumika kabla ya kusafirishwa kuja nchini.
Katika kipindi cha Serikali ya awamu ya sita jumla ya shehena za bidhaa 153,159 zilikaguliwa kabla ya kuingia nchini kupitia mfumo wa Pre-Shipment to Conformity (PVoC) na shehena za bidhaa 352,103 zilikaguliwa baada ya kufika nchini
Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa wafanyabiashara Kariakoo, Severini Mushi amesema mbali na udhibiti huo, lakini ni vyema kuhakikisha elimu inatolewa kwa wananchi ili wasiendelee kutumia bidhaa zisizothibitishwa.
Sauda Mkemi, mfanyabiashara wa vipodozi alipongeza jitihada hizo akisema zitasaidia kuokoa maisha ya watu kwa kulinda afya zao.
Ili kuhakikisha ubora unazingatiwa, Dk Katunzi amesema Serikali kupitia TBS imeanza ujenzi wa maabara katika mikoa ya kimkakati ya ambayo ni Dodoma na Mwanza utakaogharimu Sh36.802 bilioni na Sh12.078 bilioni, mtawalia.
Amesema kwa upande wa Dodoma, maabara zitakazojengwa zitahudumia mikoa mıtatu ya Kanda ya Kati ambayo ni Dodoma, Singida na Tabora, huku maabara za Mwanza zinatarajiwa kuhudumia mikoa sita, ambayo ni Mwanza, Kagera, Mara, Geita, Shinyanga na Simiyu.
“Pia, Shirika limeshapata Mshauri Mwelekezi (Consultant) wa kuchora michoro ya jengo pamoja na kusimamia ujenzi wa maabara na ofisi jijini Arusha. Hatua hiyo ya ujenzi wa maabara itasaidia kusogeza huduma karibu na wananchi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa majibu ya vipimo vya sampuli,” amesema Dk Katunzi.
Hili linafanyika wakati ambao Sh9.8 bilioni zimetumika kwa ajili ya kuimarisha ofisi tisa za kanda ambazo ni Arusha, Mwanza, Mtwara, Dar es Salaam, Dodoma, Kigoma, Mbeya, Pwani na Geita pamoja na ofisi za mipaka ya Tunduma, Kasumulo, Horohoro, Holili, Tarakea, Namanga, Bandari ya Mwanza na viwanja vya ndege.