Uchaguzi wa Malawi: Chakwera, Mutharika wajitangazia Ushindi

Lilongwe. Vyama viwili vikuu vya siasa nchini Malawi, Democratic Progressive Party (DPP) na Malawi Congress Party (MCP), vimejitangazia ushindi licha ya matokeo rasmi kutoka Tume ya Uchaguzi ya Malawi (MEC) yakiendelea kusubiriwa.

MCP, ambacho ni chama tawala, mgombea wake wa urais ni Rais Dk Lazarus Chakwera, anayetetea kiti hicho kwa muhula wa pili, na mgombea wa chama cha upinzani cha DPP, Profesa Peter Mutharika.

Kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, wakati Mutharika akitetea muhula wa pili, alishindwa na Chakwera. Mahasimu hao wanakutana kwa mara ya pili huku Chakwera akitetea kubaki madarakani.

Uchaguzi wa Malawi ulifanyika Jumanne, Septemba 16, 2025, huku idadi ya wagombea urais ikiwa 17, miongoni mwao ni Chakwera, Mutharika, na Rais wa zamani Joyce Banda.

Hata hivyo, Jumatano wiki hii, chama tawala cha MCP kilitoa taarifa kikisisitiza ushindi wa kishindo kwa Chakwera, kikisifu wapigakura kwa kuendesha uchaguzi kwa amani na kikisisitiza tena dhamira ya chama kwa misingi ya kidemokrasia.

“Ujumbe kutoka kwa wananchi unasikika wazi na kwa nguvu. Wanaamini katika maono ya Lazarus McCarthy Chakwera na maeneo matano ya kipaumbele ambayo ndiyo msingi wa ajenda yetu ya maendeleo,” amenukuliwa msemaji wa MCP, Jessie Kabwila.

Amewahimiza wafuasi kuwa watulivu, akisema: “Washindi hawasababishi vurugu, wanasherehekea kwa amani na heshima.”

Hata hivyo, tamko hilo limepingwa na msemaji wa chama cha upinzani cha DPP, Shadric Namalomba, akidai limetolewa mapema huku akimshutumu Chakwera kwa kukataa kukubali kushindwa.

“Wananchi wa Malawi wamesema, na wamesema kwa uwazi. Peter Mutharika ndiye chaguo la Wamalawi. Chakwera anapaswa kung’atuka na kuheshimu matakwa ya wananchi.”

Matokeo yasiyo rasmi yanayosambaa kwenye vyombo vya habari vya ndani na mitandao ya vyama vya siasa yanaonesha kuwa mgombea urais wa DPP, Mutharika, anaongoza katika maeneo kadhaa, yakiwemo miji mikuu na wilaya zinazojulikana kuwa ngome za MCP.

Hata hivyo, kwa mujibu wa sheria za Malawi, MEC ndiyo yenye mamlaka ya kutangaza matokeo na tayari imetoa taarifa kuwa haitaharakisha mchakato wa kutangaza matokeo wala kukubali shinikizo la kisiasa.

Kwa mujibu wa sheria, MEC inatakiwa kutangaza matokeo ya urais ndani ya siku nane, ya ubunge ndani ya siku 14, na ya serikali za mitaa ndani ya siku 21.

Pia, kwa mujibu wa sheria za uchaguzi za Malawi, mshindi wa urais ni lazima apate zaidi ya asilimia 50 ya kura halali zilizopigwa.

Chakwera ambaye ni mchungaji wa kiinjili na Mutharika ambaye ni profesa wa zamani wa sheria, wanakabiliwa na tuhuma za upendeleo na ufisadi.

Hata hivyo, wachambuzi wa kisiasa wamesema hakuna mgombea mwingine kati ya hao 17, wakiwemo Rais wa zamani Joyce Banda, ambaye ndiye mwanamke pekee katika kinyang’anyiro hicho, aliyefanikiwa kuvunja nguvu ya wawili hao wanaoongoza kwa kupata kura nyingi.

Chakwera (70) ni Rais anayemaliza anayemaliza muda wake na kutetea kwa muhula wa pili. Aliingia madarakani mwaka 2020 baada ya Mahakama kuamuru kurudiwa kwa uchaguzi wa 2019 kutokana na dosari zilizojitokeza.

Tangu aingie madarakani, Malawi kwa zaidi ya miaka mitatu imekumbwa na mfumuko wa bei na uhaba wa mafuta na dawa.

Katika kampeni zake, Chakwera amekiri kuwa hali ya uchumi si nzuri, lakini amelaumu majanga ya asili kama vimbunga na ukame uliokumba eneo hilo.

Mutharika (85) alikuwa Rais kati ya mwaka 2014 hadi 2020, aliposhindwa na Chakwera. Ni profesa wa zamani wa sheria, na anajipigia debe kwa hoja kuwa hali ya maisha ilikuwa bora wakati akiwa madarakani.

Anasifiwa kwa kushusha mfumuko wa bei na kuboresha miundombinu kama barabara wakati wa utawala wake wa kwanza. Hata hivyo, anakabiliwa na tuhuma za kuruhusu ufisadi kushamiri, madai ambayo ameyakana.

Banda (75) alikuwa Rais wa kwanza mwanamke wa Malawi, alitawala kuanzia 2012 hadi 2014. Aliingia madarakani baada ya kifo cha ghafla cha Rais aliyekuwepo, Bingu wa Mutharika (kaka wa Peter Mutharika).

Wakati wa uongozi wake, ulifichuka sakata la “Cashgate,” ambapo mamilioni ya dola yaliibwa serikalini. Banda alikanusha kuhusika na sakata hilo na tangu hapo amekuwa akijaribu kurejea tena kwenye siasa.

Usi (56) ni mchekeshaji wa zamani ambaye kwa sasa ni Makamu wa Rais wa Malawi. Alipewa nafasi hiyo baada ya kifo cha aliyekuwa Makamu wa Rais, Saulos Chilima, aliyefariki dunia kwenye ajali ya ndege mwaka jana.

Kabambe (51) ni gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Malawi. Amejaribu kuwashawishi wapigakura kwa ahadi ya kuimarisha uchumi.

Muluzi (47) ni mtoto wa Rais wa zamani Bakili Muluzi, aliyeongoza nchi kati ya 1994 na 2004. Amehudumu kama waziri katika Serikali za Joyce Banda na Peter Mutharika.

Imeandikwa na Noor Shija kwa msaada wa mtandao.