Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila imezindua Kliniki Maalumu (Premier Kliniki) ikiwa ni kuitikia kwa vitendo dhana ya tiba utalii nchini kwa kujenga miundombinu wezeshi kutoa huduma za kimataifa, kwa faragha na ubora unaokidhi viwango vya kimataifa.
Akizindua kliniki hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila amesema kuanzishwa kwa kliniki hiyo ni kutokana Serikali ya Awamu ya Sita kufanya uwekezaji mkubwa ambao umechochea viongozi kuwa wabunifu na kuanzisha huduma zingine ambapo hapo awali zilikuwa zinapatikana katika mataifa yaliyoendelea.
Mhe. Chalamila ameongeza kuwa pamoja na uanzishwaji wa huduma za kliniki maalumu, Serikali imeendelea kuboresha huduma za afya kuanzia ngazi za msingi hadi Hospitali za Rufaa na Taifa kwa kujenga na kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya, kusomesha wataalam, kuongeza bajeti ya dawa pamoja na kununua vifaa tiba vya kisasa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji MNH Dkt. Delilah Kimambo amesema kliniki hiyo inalenga kuwahudumia Watanzania, kuvutia wagonjwa kutoka ukanda wa Afrika Mashariki, kati na hata nje ya Bara la Afrika ambapo imejikita katika misingi mitatu ikiwemo ubora wa huduma, ufanisi na ubunifu kwa kutumia teknolojia za kisasa na mifumo ya kimataifa.
Naye Mwakilishi wa Bodi ya Wadhamini MNH Dkt. Khadija Malima ameahidi bodi hiyo kuendelea kuisimamia hospitali hiyo ili kuhakikisha ubora wa huduma unadumu na kuendelea kujenga imani wananchi na wageni kutoka nje ya nchi.
Akiongea kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Mratibu wa Tiba Utalii Dkt. Asha Mahita ameseama kutokana na kuimarika na kuaminika kwa huduma za afya zinazotolewa nchini watu wengi kutoka nje ya nchi kuja kupata huduma za uchunguzi na matibabu nchini sambamba na wataalam wa ndani kwenda kufanya kambi za matibabu katika mataifa hayo.