EU yaweka mkakati kuinua kilimo Tanzania

Moshi. Umoja wa Ulaya (EU) umeanzisha mpango maalumu wa kuimarisha ushirikiano wake na Tanzania katika sekta ya kilimo, ukiweka msisitizo kwenye maendeleo endelevu ya kidijitali, mabadiliko ya tabianchi na kuongeza thamani ya mazao ya bustani na kilimo ikolojia.

Kupitia mpango huo, EU itashirikiana na Serikali ya Tanzania pamoja na wadau mbalimbali kutathmini fursa za uwekezaji na kusaidia wakulima kwa teknolojia rafiki kwa mazingira, ikiwa ni sehemu ya ajenda ya maendeleo jumuishi.

Akizungumza leo katika Manispaa ya Moshi, wakati wa ziara ya mabalozi 12 kutoka nchi wanachama wa EU katika kiwanda cha viuatilifu vya asili cha Pant Biodefenders Limited, kiongozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Christine Grau amesema ziara hiyo ya siku tatu inalenga kutembelea miradi inayosaidia wakulima, wanawake, vijana na wajasiriamali wadogo .

“Ziara hii ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya ushirikiano kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya, na miaka 25 ya ushirikiano kati ya EU na Umoja wa Afrika, ni fursa ya kuona matokeo halisi ya miradi ya EU kwa wakulima, wajasiriamali na wabunifu wa ndani,” amesema Grau.

Miongoni mwa mabalozi 12 wa Umoja wa Ulaya(EU) wakiwa katika kikao cha pamoja kujadili masuala mbalimbali ya kilimo, Mkoani Kilimanjaro.

Amesema  kuwa,  EU na nchi wanachama wake wamejipanga kuimarisha uzalishaji, uendelevu na ustahimilivu wa sekta ya kilimo nchini Tanzania, hususan katika mazao ya kimkakati kama kahawa.

Amesema kuwa EU imezindua mkakati wa Global Gateway, unaolenga kuendeleza miundombinu ya kidijitali, nishati, usafiri, pamoja na kuboresha mifumo ya afya, elimu na utafiti barani Afrika na duniani kote.

Mkurugenzi Mtendaji wa Pant Biodefenders Limited, Dk Never Mwambela amesema ujio wa mabalozi hao umefungua fursa kubwa kwa wakulima na wasindikaji nchini, hasa kwa bidhaa zinazolenga masoko ya kimataifa.

“Nchi za EU hazitaki mabaki ya sumu kwenye mazao kama kahawa, parachichi na mazao mengine ya chakula, hivyo, kwa kutumia viuatilifu vya asili, tunalinda afya ya wakulima na kuwasaidia kufikia viwango vya kimataifa vya ubora wa mazao,” amesema Dk Mwambela.

“Tunahitaji kufika kila kijiji kutoa elimu na viuatilifu bure kupitia miradi hii, zao la kahawa limeathiriwa sana, miti imekufa, mchwa wameshambulia na wakulima wengi wamekata tamaa, tunaamini kupitia ushirikiano huu mpya, hali itabadilika,” amesema.