Soud aahidi kuondoa ushuru bandarini, karafuu kuuzwa Sh50,000 akitinga Ikulu

Unguja.Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wakulima (AAFP), Said Soud Said amesema endapo atachaguliwa kuingia Ikulu, kilo moja ya karafuu itauzwa Sh50,000 ili kuhakikisha wakulima wananufaika na zao hilo.

Akizungumza leo Alhamisi Septemba 18, 2025 katika uwanja wa Mabembea Malindi Mkoa wa Mjini Magharibi wakati wa kampeni za chama chake, Soud pia ameahidi bandari ya Zanzibar itakuwa bure kuingiza mizigo, kwa kuwa tozo zinazotozwa sasa ni kubwa kuliko thamani ya bidhaa zinazoingizwa.

“Inasikitisha kuona mkulima wa karafuu hana hata baiskeli, lakini mnunuzi wa karafuu anaendesha gari aina ya Prado. Huu ni unyonyaji, naomba mnipeleke Ikulu ili tupate ufumbuzi wa changamoto hizi,” amesema.

Akigusia suala la bandari, amesema endapo atapata ridhaa, Zanzibar itakuwa freeport, ili kupunguza gharama kubwa za ushuru wa bidhaa.

“Ukienda Dubai unaweza kununua gari kwa Dola 150 za Marekani lakini likifika katika bandari yetu unalipia ushuru wa zaidi ya Dola 6,000. Hali hii haiwezi kuendelea,” amesema mgombea huyo wa urais wa Zanzibar.

Amesema vijana wanashindwa kuwapelekea wazazi wao zawadi kutokana na gharama hizo kubwa na ameahidi kubadili mifumo ili vijana wamiliki magari badala ya kubaki kwenye bodaboda.

Aidha, amesema iwapo atachaguliwa kazi za vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) zitakuwa ni kulima karafuu na minazi, huku jukumu la ulinzi likibaki kwa Jeshi la Polisi pekee.

“Vikosi vitajikita kulima karafuu na minazi ili kuboresha mazao haya. Mambo ya kuzurura mitaani yakiambatana na kuvaa mashati yataisha. Polisi pekee wanatosha kwa ulinzi,” amesema.

Soud pia amewaomba vijana kumpigia kura kwa wingi, akiahidi kuwatafutia njia za kujipatia vipato na kuongeza furaha.

“Kwa sasa vijana hawana sehemu ya kustarehe, badala yake wanaona Forodhani ndiyo sehemu pekee ya kustarehe. Nitabadili hali hii,” ameahidi.

Mgombea huyo amewataka wazazi kupunguza mahari kwa kuwa kiwango kikubwa kimekuwa kikwazo kwa vijana kuoa.

Amerejea kauli yake kwamba akichaguliwa atapiga marufuku vitanda vya futi sita kwa sita, akidai vinachangia wanandoa kutopata watoto kutokana na kutokaribiana.

Awali, akiwatambulisha wagombea wa ubunge na uwakilishi wa Malindi kupitia AAFP, Soud amesema wana uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko ya kimaendeleo.

“Tumeona Bunge lililopita likiwa na watu waliokuwa kimya, mithili ya mabubu. Mkipeleka watu wa aina hiyo, Rais hatakuwa na mtu mwenye uwezo wa kuteua, na mwisho wa siku mtalalamika,” amesema.

Kwa upande wake, mgombea uwakilishi wa Malindi, Hafidh Othman Jabu amesema licha ya maendeleo ya kitaifa yaliyofanyika katika kipindi cha miaka mitano, jimbo hilo limekosa mafanikio kutokana na kukosa viongozi wenye uwezo wa kuyasimamia.

Naye mgombea ubunge wa jimbo hilo kupitia chama hicho, Said Kheri Ame amesema Malindi lina fursa nyingi ikiwemo ya bandari, lakini limekosa watu sahihi wa kuzitumia.

Hivyo, ameahidi wakipatiwa ridhaa watahakikisha fursa hizo zinatumiwa kwa manufaa ya wananchi.

Awali, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Omar Juma Said aliwataka wananchi kutoongozwa na mihemko ya kisiasa wakati wa kuchagua viongozi.

“Tuache kuchagua kwa mihemko, badala yake tuzingatie kulinda amani na umoja wetu,” amesema.