Dodoma. Kuna usemi usemao haijaisha mpaka iishe, ndio unaweza kuutumia kuelezea harakati za Luhaga Mpina kuendelea kupigania haki yake ya kuteuliwa na Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) kuwania urais kwa tiketi ya Chama cha ACT Wazalendo.
Kinachoendelea kwa sasa baina ya Mpina na INEC ni kama filamu ambayo kila mdau wa siasa na wananchi kwa ujumla, anasubiri kuona mwisho wake.
Kwa sasa Mpina na ACT-Wazalendo wamefungua shauri lingine Mahakama Kuu, kupinga kuenguliwa kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu 2025.
Maombi hayo namba 23617 ya 2025 yamefunguliwa katika Masjala Kuu ya Mahakama Kuu Dodoma yakiambatanishwa na hati ya usikilizwaji wa haraka (extreme urgency), huku kampeni zikiingia siku ya 22 Septemba 18, 2025.
Safari hii, Bodi ya Wadhamini ACT Wazalendo na Mpina wamefungua maombi dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), na yamepangwa kusikilizwa Septemba 22, 2025 mbele ya Jaji Wibert Chuma.
Kwa mujibu wa mwenendo wa shauri hilo uliopo katika mfumo wa e-Services Portal wa Mahakama, kesi hiyo imepangwa kusikilizwa Jumatatu Septemba 22,2025 na pande zote za shauri hilo wametakiwa kuwapo mahakamani.
ACT Wazalendo na Mpina wanaomba amri nne, moja ni kupewa kibali cha kufungua maombi ya kuomba kubatilishwa kwa uamuzi wa Msajili wa vyama vya siasa wa kumwengua Mpina kuwa mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu 2025.
Ombi la pili ni kupatiwa kibali cha kufungua maombi kubatilisha barua ya msajili wa vyama vya siasa ya Agosti 26, 2025 na kutamka kuwa maudhui ya barua hiyo yasifanyiwe kazi na taasisi yeyote kuhusiana na haki ya Mpina kugombea urais.
Mbali na ombi hilo, anaiomba mahakama itoe kibali hicho ili kufungua maombi ya kupata amri ya mahakama ya kuwazuia Msajili na AG, kuingilia haki ya Mpina kugombea nafasi ya urais, hadi pale uamuzi wa maombi hayo utakapotolewa.
Lakini mahakama itoe amri yeyote itakayoona inayofaa kuhusiana na shauri hilo ambapo ni la pili kufunguliwa na waleta maombi hao, baada kushinda shauri la kwanza dhidi Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na AG kupinga kutomteua kugombea.
Mpina alipitishwa na Mkutano Mkuu wa ACT -Wazalendo wa Agosti 6,2025 kugombea urais kupitia chama hicho, lakini Msajili akatangaza kubatilisha uteuzi huo kutokana na pingamizi lililowekwa na kada wa chama hicho, Monalisa Ndala.
Ndala katika pingamizi lake, alidai kuwa uteuzi wa Mpina ni batili, hakuwa na sifa kwa mujibu wa kanuni za kudumu za uendeshaji wa chama hicho toleo la mwaka 2015, ambapo msajili aliiandikia INEC kutopokea fomu za uteuzi za Mpina.
Bodi ya Wadhamini na Mpina walifungua kesi Agosti 27, 2025 kupinga uamuzi huo wa INEC ambapo Septemba 11, 2025 mahakama ilikubali maombi ya Mpina na kuiamuru INEC ipokee fimu zake na iendelee na mchakato wa uteuzi ulipoishia.
Mahakama ilieleza kuwa uamuzi wa INEC kumzuia Mpina kurejesha fomu za uteuzi Agosti 27, 2025 bila kupewa haki ya kusikilizwa ulikuwa unakinzana na ibara ya 13(6)(a) ya Katiba ya nchi kwa kutompa haki ya kusikilizwa kwa mujibu wa Katiba.
Septemba 13, 2025, Mpina alirejesha fomu zake na INEC kumteua kugombea urais, lakini uteuzi huo ulidumu kwa saa chache kwani aliwekewa pingamizi na wagombea wenzake wawili na AG na INEC ikalikubali pingamizi lililowekwa na AG.
Katika maelezo yao ya pamoja katika kesi mpya iliyofunguliwa Septemba 15, 2025 kupitia kwa Wakili John Seka na Edson Kilatu, Bodi ya Wadhamini na Mpina, wanadai Msajili alitafsiri vibaya Katiba ya ACT – Wazalendo na Kanuni zake.
Ni kutokana na kutafsiri huko vibaya, kulisababisha kuondolewa kwa mleta maombi wa pili (Mpina) kuwa mgombea urais kwa tikei ya chama hicho na kwamba Msajili alitumia vibaya mamlaka yake kufuta uteuzi wa Mpina.
Waleta maombi wanaeleza kuwa mjibu maombi wa kwanza (Msajili) alikiuka msingi wa haki ya kusikilizwa (natural justice) kwa kumwengua Mpina kwenye kinyang’anyiro cha urais bila kumsikiliza na kuathiri haki yake ya kugombea.
“Mjibu maombi wa kwanza alitumia mamlaka yake ya kisheria ya kufuatilia uchaguzi wa ndani wa vyama chama kwa madhumuni yasiyofaa ya kumwengua mwombaji wa pili (Mpina) kwenye kinyang’anyiro cha urais,” wanadai.
Kupitia maelezo hayo ya pamoja, Bodi ya Wadhamini na Mpina, wanaeleza kuwa mjibu maombi wa kwanza ambaye ni Msajili alitenda kinyume cha sheria, bila mantiki, na kwa nia mbaya alipobatilisha uteuzi wa muombaji huyo wa pili.
“Hii inadhihirika kwa sababu mwakilishi wa mjibu maombi wa kwanza ambaye alikuwepo mkutanoni na ambaye aliidhinisha mchakato huo, hakuwahi kuleta pingamizi lolote kwa uteuzi wa mwombaji wa pili,” wanadai wajibu maombi.
“Mlalamikiwa wa kwanza alimwondolea sifa mwombaji wa pili bila kusikilizwa, kwa sababu zisizo na msingi na za nje, licha ya uteuzi wake kuwa unazingatia kikamilifu katiba na kanuni za chama (ACT Wazalendo),” wamesisitiza.
Viapo vya Ruhwanya, Mpina
Mleta maombi wa kwanza kupitia kiapo cha Mhonga Ruhwanya ambaye ni mmoja wa wadhamini wa ACT-Wazalendo, anaeleza kuwa Katiba ya ACT Wazalendo, Kanuni toleo la 2025 na miongozo, mgombea urais anateuliwa na mkutano mkuu.
Ameeleza kuwa kifungu cha 4(a), (b) na (c) cha muongozo wa ndani wa uteuzi wa wagombea kwenye Uchaguzi Mkuu 2025 umetaja sifa inayotakiwa na ACT -Wazalendo kwa mtu anayetaka kudhaminiwa na chama hicho kugombea, ikiwamo kiti cha urais.
“Kwa hakika, chini ya masharti yaliyotajwa hapo juu, hakuna hitaji la muda wa uanachama kwa nafasi ya mgombea urais anayefadhiliwa na mwombaji wa kwanza (ACT – Wazalendo),” ameeleza mjume huyo wa bodi ya wadhamini.
Kwa mujibu wa Ruhwanya, Julai 29, 2025, Mpina alijiunga na ACT – Wazalendo kama mwanachama na alipewa usajili kupitia mifumo (portal) ya chama hicho na baadaye alionyesha nia ya kudhaminiwa na chama hicho kugombea urais.
“Jina lake na la Aaron Kalikawe yalifanyiwa kazi kulingana na taratibu za chama na kupelekwa mkutano mkuu maalum uliofanyika Agosti 6, 2025 kwa ajili ya kupigiwa kura chini ya usimamizi wa Naibu Msajili kutoka ofisi ya Msajili,” anaeleza.
“Mleta maombi wa pili alipata kura nyingi na alitangazwa kuwa ameshinda na kuteuliwa na jina lake lilipelekwa INEC kwa ajili ya kuchukua fomu za uteuzi kuwania kiti cha urais cha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” anasema.
Katika mchakato wa uteuzi, Ruhwanya anaeleza kuwa mleta maombi wa kwanza alipokea barua kutoka kwa Msajili ikitaka maelezo kuhusiana na utaratibu uliotumika kumteua mleta maombi wa pili ambaye ni Luhaga Mpina.
Kwa mujibu wa Ruhwanya, walijibu barua hiyo na kuthibitisha kuwa uteuzi wake ulizingatia Katiba ya chama hicho, kanuni na miongozo ya chama lakini Agosti 26,2025, Msajili akatoa barua akimwengua mleta maombi wa kwanza.
Kwa upande wake, Mpina katika kiapo chake, maudhui yake hayatofautiani sana na ya Ruhwanya ambapo alielezea kwa kirefu safari ya kujiunga kwake ACT – Wazalendo na namna alivyochaguliwa kuwa mgombea urais kwa uwazi.
Hata hivyo, anasema anafahamu kuwa Agosti 26, 2025, Msajili wa Vyama vya Siasa aliwaandikia barua waleta maombi wa kwanza akiwajulisha kuenguliwa kwake na anafahamu ni barua hiyo hiyo, ndio iliyonakiliwa kwenda Tume ya Uchaguzi.
Ni kutokana na barua hiyo, Mpina anasema alizuiwa na INEC kurejesha fomu za uteuzi nafasi ya urais na akafungua shauri namba 21692/2025 kupinga ambapo Mahakama iliona alidhulumiwa haki yake kwa kuadhibiwa bila kusikilizwa.
Lakini anasema kwa sasa amezuiwa na INEC kugombea nafasi ya urais wa Tanzania utakaofanyika Oktoba 29, 2025 wakiegemea uamuzi huo wa Msajili wa vyama na kwamba sasa wameamua kufungua maombi hayo ya mapitio ya mahakama kuupinga.