TUME YA TAIFA YA MIPANGO YAANZA MIKAKATI UKELEZAJI DIRA YA TAIFA 2050

Na Seif Mangwangi, Arusha.

TUME ya Taifa ya Mipango imeanza mikakati ya utekelezaji wa mpango wa nne wa Taifa wa miaka mitano kwa kukutanisha wataalam wa utafiti, ubunifu na tathmini kutoka taasisi za kimkakati zaidi ya 100 za Serikali, asasi binafsi za maendeleo za ndani na nje ya nchi na vyuo vikuu.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi hicho leo Septemba 18, 2025 jijini Arusha, Naibu Katibu Mtendaji biashara na ubunifu wa  Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt Blandina Kilama amesema baada ya kuzinduliwa kwa Dira ya Taifa 2050, Tume hiyo inapaswa kuweka mikakati ya namna ya kufanya tafiti mbalimbali ili kupata vipaumbele vya Taifa vitakavyofanyiwa kazi kwa miaka mitano ijayo.

Amesema katika kikao hicho cha saa 36 wataalam hao watatengeneza ajenda za utafiti kutokana na vipaumbele vya jamii ambayo itatumika kwa miaka mitano ya utekelezaji wa dira ya Taifa lakini pia watatumia kikao hicho kuweka mikakati ya kutafuta fedha zitakazotumika kwenye utafiti  kwa miaka mitano ya utekelezaji wa ajenda hiyo ya kitaifa.

“ Baada ya wataalam hawa kusaidia kutengeneza vipaumbele vya miaka mitano katika utafiti, pia watatengeneza vipaumbele ambavyo vitatekelezwa kwa mwaka mmoja mmoja, hii ndio kazi ya Tume ya Taifa ya mipango na yote haya tunayadadavua kutoka kwenye dira ya Taifa ya 2050,”amesema.

Dkt Blandina amesema baada ya kukamilika kwa ajenda hiyo na kukabidhiwa serikalini kwaajili ya utekelezaji wake ambapo inatarajia kuanza kufanyakazi rasmi mwakani Julai 2026, tume ya Taifa ya mipango itaendelea kufuatilia utekelezaji wa mipango hiyo ili kubaini hatua iliyofikiwa na kama kuna mkwamo wowote wa utekelezaji wake wataalam wa tume hiyo watapaswa kufanya utafiti kujua tatizo ni nini.

Kwa upande wake Dkt. Linda Ezekiel amesema mbali ya kikao hicho, pia kuna wataalam zaidi ya 30 wako Jijini Dar es salaam wakipitia dira ya Taifa 2050 kudadavua vipaumbele vya jamii ambavyo vitaenda kufanyiwa kazi kwa miaka mitano ijayo kwa vipindi vitano vitano.

Aidha amesema pamoja na uwepo wa Dira hiyo pia tume ya mipango imekuwa ikitengeneza mipango yake kwa kuzingatia mabadiliko yanayoendelea kutokea duniani ikiwemo kukua kwa teknolojia na athari ambazo zimekuwa zikisababishwa na mabadiliko ya tabia nchi.

 “Tukiwa hapa kwa saa 36 lazima wataalam hawa watokea na suluhu ya kujua pesa za kufanyia utafiti kuhusu utekelezaji wa dira ya Taifa zitatokea wapi kwa kuwa huwezi kufanya utafiti bila ya kuwa na fedha, lakini wao ni wataalam watajua na ndio sababu tumekutana hapa watu kutoka sekta mbalimbali za kimkakati,”amesema.

Mkurugenzi wa utafiti na mafunzo kutoka shirika la utafiti la REPOA, Lucas Katera anasema shirika lake limekuwa likifanya tafiti mbalimbali kusaidiana na Serikali katika utekelezaji wa ajenda za maendeleo hivyo wamealikwa katika kikao hicho ili kuweza kudadavua namna ya kutekeleza dira ya Taifa ya 2050 katika idara ya tafiti na ubunifu lakini pia namna ya kupata fedha za kuendeshea tafiti hizo.

Kwa upande wake Mkuu wa programu kutoka shirika la maendeleo la UNDP, Emmanuel Nnko amesema ni muhimu kwa tume ya taifa ya mipango kutengeneza ajenda za utafiti pamoja na kujua namna pesa ya tafiti hizo itakapopatikana ili kuwezesha utekelezaji wa dira ya Taifa2050.

Amesema hivi sasa Tanzania inaingia kwenye uchumi wa kati hivyo masharti nafuu ambayo ilikuwa ikiyapata kutokana na mikopo mbalimbali yataondolewa Kwa kuwa itakuwa katika nchi zinazojiweza kiuchumi.