Mwanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe adaiwa kuuawa kwa kuchomwa moto, Polisi yaanza uchunguzi

Mbeya. Wakati taharuki ikitanda jijini Mbeya kuhusu kifo cha aliyekuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza Chuo Kikuu Mzumbe ndaki ya Mbeya, Shairose Mabula anayedaiwa kuawa  kwa kuchomwa moto na wasiojulikana, Jeshi la Polisi mkoani humo limesema linaendelea na uchunguzi juu ya tukio hilo. 

Taarifa ya tukio la kuuawa kwa mwanafunzi huyo zilianza kusambaa leo Alhamisi Septemba 18,2025 katika mitandao ya kijamii na kuzua taharuki na sintofahamu kutokana na utata wa mazingira ya kifo hicho. 

Katika taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya leo imeeleza  kuwa Septemba 14,2025 Baba mzazi wa marehemu huyo, Michael Mabula alifika kituo kikuu cha Polisi Mbeya kutoa taarifa ya kupotea kwa binti yake. 

Taarifa hiyo imeeleza kuwa  baada ya kupokea taarifa hiyo, Jeshi hilo lilifungua jalada la uchunguzi na ufuatiliaji ili kumpata, ambapo Septemba 16, saa 5:00 usiku lilipokea taarifa za ajali ya moto katika mtaa wa Moravian Kata ya Isyesye. Kufuatia taarifa hiyo  askari Polisi walikwenda eneo la tukio na kukuta kibanda kikiteketea kwa moto. 

“Baada ya uchunguzi ilibainika kuna mwili wa mtu mmoja jinsia ya kike unaungua ambao kwa wakati huo hakuweza kutambulika, ambapo mwili huo ulichukuliwa na kuhifadhiwa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya,”imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

“Baada ya uchunguzi wa kitabibu na kuhusisha ndugu, ilibainika kuwa mwili huo ni wa Shairose Mabula aliyekuwa anatafutwa baada ya kuripotiwa kupotea, Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kisayansi ili kutambua mwili wa marehemu na kuwakamata waliohusika na mauaji” Imeeleza taarifa hiyo. 

Hata hivyo taarifa hiyo imeeleza kuwa linatoa wito kwa yeyote mwenye taarifa zitakazofanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa, huku likilaani tabia ya kujichukulia sheria mkononi na kusababisha madhara makubwa kwa jamii. 

Kauli ya baba wa marehemu

Akizungumza nyumbani kwake mtaa wa uzunguni jijini Mbeya, Dk Mabula Mahande amesema alipata taarifa kupitia simu za watekaji wakimwambia wanambeba mwanaye kwenda Tabora, ambapo aliwauliza kuna tatizo gani wakamuahidi kumjibu baadaye. 

Amesema kuwa ilipofika muda wa takribani saa 5 usiku, mmoja wa wasamaria wema alitoa taarifa za kuwapo moto katika eneo la Nanenane kuwa kuna vibanda vinawaka moto ndio zimamoto walifika kuuzima. 

“Waliniuliza fulani unamfahamu (wakataja jina lake) nikasema ndio ni mwanangu wakaniambia wanaenda naye Tabora nikauliza kuna tatizo gani wakasema wataniambia baadaye,” Amesema na kuongeza 

“ilipofika saa 4 hadi 5 hivi usiku kulioneka kuzuka moto kule Nanenane na mmoja wa wasamaria wema akapiga simu Zimamoto ile wanazima wakaona kuna mwili unaungua” Amesema Dk Mabula.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Uzunguni, Kelvin Mela amesema alipokea taarifa za kupotea kwa marehemu huyo kutoka kwa baba yake mzazi ambaye walishirikiana kwa hatua zote hadi kuthibitika kupatikana kwake akiwa amefariki. 

“Tangu kupotea kwake aliniambia hadi tukaenda kutoa taarifa za kutekwa kwa mwanaye hadi ilipothibitika na kupatikana akiwa amefariki, ikumbukwe baba yake mzazi alikuwa amesafiri” amesema Mela. 

Naye mmoja wa wanafunzi aliokuwa akifanya nao masomo yake kwa vitendo (Field) katika Mahakama ya mwanzo Mbeya mjini, Ezekiel Mwakalebela amesema marehemu alikuwa mpole na mwenye ushirikiano akieleza kuwa ni masikitiko kwa tukio lililomkuta. 

“Kwanza ilitushtua na kutusikitisha, kwa kuwa tulikuwa naye field hapa Mahakama ya mwanzo akitokea chuo kikuu Mzumbe, alikuwa mpole na mwenye ushirikiano, kifo chake kimetushtua na kutusikitisha,”mesema Mwakalebela.