ONA itakavyounganisha Afrika Mashariki, kushusha gharama za mawasiliano

Arusha. Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imeanza jitihada za kupanua mfumo wa mtandao wa pamoja (ONA) kwa kuunganisha huduma zinazoendeshwa kwa misingi ya takwimu.

Lengo la mfumo huo ni kwa ajili ya kuboresha mawasiliano ya kikanda na kupunguza gharama za huduma ya mtandao kusafiri (roaming) miongoni mwa nchi wanachama.

Upanuzi wa ONA unatarajiwa kujumuisha teknolojia mpya zinazoibuka kama vile e-SIMs, IoT roaming, na huduma zinazotumia takwimu.

Mfumo huu inaoakisi mabadiliko yanayoendelea katika mawasiliano ya kidijitali unapendekezwa na Mradi wa Kikanda wa Ujumuishaji Kidijitali wa Afrika Mashariki (EARDIP).

Mradi huu unalenga laini ya simu hiyo hiyo uliyonayo nchini kwako unaweza kuwasiliano nayo kwa kupiga au kupigiwa simu, kutuma ujumbe mfupi au kutumia kifurushi chako cha bando ukisafiri kwenda nchi yoyote ya Jumuiya ya Afrika Mashariki tena kwa gharama ile ile ya ukiwa ndani ya nchi yako.

Mpango huu uliopendekezwa Agosti 2025 ndani ya kikao cha wataalamu wa mawasiliano na teknolojia EAC wametoka serikalini, wakala wa udhibiti, pamoja na kampuni za simu yalikuwa sehemu ya malengo ya mradi huo ya kukuza na kuunganisha masoko ya mawasiliano na kuimarisha mfumo wa ONA.

Mkurugenzi wa Maudhui ya Uchumi na Masuala ya Watumiaji katika Mamlaka ya Mawasiliano Uganda, Julianne Mweheire anasema mfumo wa ONA umejengwa katika misingi inayojumuisha kupunguza gharama za kuunganisha simu, kuondoa gharama za roaming, na kuweka viwango vya pamoja vya mawasiliano ya simu katika mipaka ya kanda.

Anasema upanuzi huu, unaakisi dhamira ya kanda katika mabadiliko ya kidijitali na mawasiliano yasiyo na mipaka, hatua itakayorahisisha wananchi, wafanyabiashara na taasisi mbalimbali kuendelea kuunganishwa hata wanapovuka mipaka.

“ONA ni kwa ajili ya kila mtu, mfanyabiashara anayevuka mpaka, mwanafunzi anayesoma nje ya nchi na mwekezaji anayowekeza kwenye mitandao kwani hii inafunga mapengo yaliyopo kwenye gharama na kutafungua fursa nyingi,” anasema.

“Hatua hii pia inarahisisha usafirishaji wa watu, bidhaa na huduma kupitia kuwasiliana na hivyo kuongeza biashara ya ndani ya kanda.

Dk Franklin Makokha kutoka mamlaka ya mawasiliano Kenya anasema mfumo ulioboreshwa lazima ushughulikie vitendo haramu kama vile SIM boxing, kuweka kanuni za matumizi ya haki.

“Hii ni kwa ajili ya kuzuia matumizi mabaya, kulinda watoa huduma wadogo dhidi ya kutozwa bei ya juu na watoa huduma wakubwa, na kutekeleza mekanizimu wazi za kikanda za utekelezaji,” anasema.

Meneja Mawasiliano na Intaneti kutoka mamlaka ya mawasiliano Tanzania, Fuad Adam Rwabuhungu anasema Mfumo wa roaming uliosawazishwa kikanda siyo tu kutaendesha ujumuishaji wa kikanda bali pia ni kichocheo cha ukuaji wa biashara na uchumi kwa ujumla.

Mfumo ulioboreshwa wa ONA unatarajiwa kuanzisha mifumo ya ulinzi na sera za matumizi ya haki, ili kuzuia matumizi mabaya, sambamba na kuweka mifumo thabiti zaidi ya utekelezaji wa kikanda.

Mtaalamu wa masuala ya uchumi Elias Marisa anasema kuwa Wananchi wa Afrika Mashariki wanapaswa kuwa na uwezo wa kusafiri, kufanya biashara, na kuunganishwa miongoni mwa mipaka yetu bila vikwazo vyovyote.

“Mfumo huo wa mawasiliano utazidisha maana ya ujumuishaji wetu kwani tutakuwa na uhuru wa mawasiliano bila kuwa na wasiwasi kuhusu gharama. Hii ni kuhusu kufanya ujumuishaji wa kikanda uwe halisi katika maisha ya kila siku ya watu,” anasema.

Katibu Mkuu wa Kudumu, Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia za Habari na Vyombo vya Habari, Burundi Ferdinand Manirakiza anasema kuwa mpango unatakiwa uharakishwe ili kuondoa kizuizi cha mawasiliano kilichopo sasa.

Anasema kuwa kwa sasa hakuna laini inaweza kufanya kazi ya kupiga, kutuma sms wala kutumia bando ukiwa nchi nyingine na hata wanaojitosa kupigiwa hutumia gharama kubwa kulingana na nchi aliyoko.

“Unakuwa na laini ya kampuni hii nchini kwako lakini ukienda kwenye nchi nyingine jirani tu hapo ile kampuni haikusaidii hata kuwasiliana na mtu wa laini ya kampuni hiyo hiyo, ndio maana tumeanzisha mjadala huu tukiona ndio wakati sahihi wa kuondolewa kwa vikwazo hivyo,” anasema.

Takwimu Muhimu za Mawasiliano

Kwa mujibu wa Shirika la Mawasiliano Afrika Mashariki (EACO), idadi ya usajili wa simu za mkononi katika ukanda wa EAC imefikia milioni 199.7, sawa na asilimia 100 ya uenezaji, wakati dunia ikiwa na jumla ya bilioni 8.6, uenezaji asilimia 111.

Kwa upande wa intaneti ya simu, usajili umefikia milioni 122.3, sawa na asilimia 61 ya uenezaji, huku duniani usajili ukifikia bilioni 4.6 na uenezaji ukiwa kwa asilimia 67.

Trafiki ya simu za sauti za ndani imefikia dakika bilioni 346.5, ishara ya ongezeko la matumizi ya huduma za mawasiliano.

Katika mtandao wa 2G, uenezaji wa huduma kwa wananchi ni wa wastani wa asilimia 92, ambapo Rwanda inaongoza kwa asilimia 99, ikifuatiwa na Uganda na Tanzania asilimia 98, Kenya na Burundi asilimia 97, huku Sudan Kusini ikiwa chini kwa asilimia 65.

Kwa mtandao wa 3G, uenezaji umefikia wastani ni asilimia 78, Rwanda na Kenya zikiongoza kwa asilimia 99 na asilimia 97 mtawalia, Tanzania ikiwa na asilimia 86, Uganda asilimia 78, Burundi asilimia 51 na Sudan Kusini kwa asilimia 54.

EAC yenye idadi ya watu takribani milioni 331.1, inalenga kutumia mfumo huu wa ONA kama chachu ya maendeleo ya uchumi, urahisishaji wa biashara na kuimarisha ujumuishaji wa kijamii na kidijitali.

Hili linaonekana wakati ambao takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha kuwa hadi Juni 2025 kulikuwa na watumiaji wa simu milioni 92.7 huku watumiaji wa intaneti wakiwa 54.1.

Idadi za laini za simu zilizosajiliwa zilikuwa ni ongezeko kutoka milioni 90.4 katika robo ya mwaka iliyoishia Machi 2025 ikiwa ni sawa na ongezeko la 2.6.

Takwimu hizi zinaonyesha kuwa Dar es Salaam ilishika nafasi ya kwanza kwa kuwa na laini milioni 17.07, Mwanza ilishika nafasi ya pili kwa kuwa na laini milioni 6.14, Arusha ilishika nafasi ya tatu kwa kuwa na laini milioni 5.58, Mbeya ilishika nafasi ya nne ikiwa na laini milioni 5.34 na Dodoma ilishika nafasi ya tano kwa kuwa na laini milioni 4.95.

Katika laini za simu zilizokuwapo, idadi ya dakika ndani ya nchi zilikuwa bilioni 43.3 huku idadi ya dakika kutoka nje ya nchi zikiwa ni milioni 39.8 pekee.

Wakati huohuo takwimu hizi zinaonyesha kuwa asilimia 93 ya watu nchini walikuwa wamefikiwa na kasi ya 3G nchini katika huduma ya intaneti wakati ambao watumiaji wa simu janja walikuwa ni milioni 27 pekee.

Mtaalamu wa Uchumi, Oscar Mkude anasema hatua hii itapunguza gharama za watu kupiga simu kwenda katika ukanda wa Afrika ya Mashariki bila kuwa na tozo za ziada.

“Hii itakuwa ni faida ya kwanza ya moja kwa moja na itakwenda kuchochea kuongezeka kwa watu wanaopiga simu ambao awali walikuwa wakiogopa kupiga simu kutokana na gharama zilizopo,” anasema.

Kupungua kwa gharama hizo, kutachochea kuongeza kipato cha watu kutokana na kubakiwa na akiba ya fedha ambayo awali walikuwa wakiitumia katika vocha ili waweze kufanya mawasiliano na sasa fedha hizo zitakwenda kutumika katika kufanya shughuli nyingine za kiuchumi.

“Hali kama hii sasa ina mchango mkubwa katika kuifanya jumuiya iwe imara, moja ya jambo linalofanya jumuiya kuwa imara ni kuwapo kwa mwingiliano imara wa watu na muingiliano huo ndiyo utalinda muungano uliopo hata itakapotokea jambo lolote,” anasema.