::::::::;
Na Mwandishi Wetu,
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imewataka wananchi hususan kutoka makundi yenye mahitaji maalumu kujitokeza kwa wingi kujisajili ili kupata Vitambulisho vya Taifa, hatua ambayo itarahisisha upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii ikiwamo afya, elimu na huduma za kifedha.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji Vitambulisho kutoka NIDA, Bw. Edson Guyai, wakati wa zoezi maalum la usajili kwa watu kutoka makundi maalumu, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Vitambulisho Duniani yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
“Tunaendelea na juhudi kuhakikisha kila Mtanzania anapata kitambulisho cha taifa ifikapo mwaka 2030, kama sehemu ya kutimiza malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs). Makundi maalumu kama watu wenye ulemavu wanahitaji kipaumbele ili wasiachwe nyuma katika upatikanaji wa huduma,” alisema Bw. Guyai.
Kwa mujibu wa NIDA, zoezi hilo maalum limekuwa sehemu ya mkakati wa kuhakikisha hakuna Mtanzania anayeachwa nyuma, hasa wale wanaokabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma za usajili kutokana na hali zao za kiafya au kiuchumi.
Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa ya Temeke, Bi. Ristituta Simon, alisema mwitikio wa watu wenye ulemavu katika kupata huduma hiyo bado ni mdogo, hali inayochangiwa na uelewa hafifu au ukosefu wa taarifa sahihi kuhusu umuhimu wa kuwa na kitambulisho hicho.
“Changamoto kubwa imekuwa ni uelewa mdogo au ukosefu wa taarifa sahihi miongoni mwa baadhi ya watu wenye ulemavu. Kupitia kampeni hii, tumewaelimisha na kuwawezesha wengi kupata haki yao ya msingi,” alisema Bi. Ristituta.
Naye mmoja wa wananchi waliopata huduma hiyo, Bw. Maabadi Juma, alisema kitambulisho cha taifa ni nyenzo muhimu kwa maisha ya kila siku, hasa katika kupata huduma kama za benki, hospitali na hata za elimu.
“Ni muhimu sana kwa wenzetu wenye mahitaji maalumu kujitokeza kwa wingi katika ofisi za NIDA. Kitambulisho hiki kinahitajika hata wakati wa kufungua akaunti benki au kupata huduma za matibabu,” alisema.
Mamlaka hiyo imeeleza kuwa itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha wananchi wote wanapata haki yao ya msingi ya kitambulisho, ili kuchochea ushiriki mpana wa kijamii na kiuchumi katika taifa.















