Kisukari, shinikizo la damu: Magonjwa yanayoua kimyakimya

Dar es Salaam. Ni maadui wawili wakubwa wa uhai wa binadamu. Aghalabu wanakuja kimya kimya bila onyo.

Utapata  maumivu ya kichwa utachukulia sawa na  msongo wa mawazo. Uchovu utasema pengine ni kwa sababu ya kufanya kazi sana kila siku. 

Ukiwa na jeraha hata dogo litachukua miezi  kupona. Kwa mamilioni ya watu duniani, dalili hizi zinaonekana kuwa rahisi na zisizo na tishio lolote lakini wasichojua wengi, hizi ni dalili zinazoficha magonjwa mawili hatari zaidi katika wakati wetu ambayo ni kisukari na shinikizo la damu.

Unaweza kuyaita “wauaji wa kimyakimya,” kwani  yanaweza kukuua bila kugundulika kwa miaka mingi. 

Kibaya zaidi pale yanapogundulika, wagonjwa wengi huwa  tayari wanakabiliana na madhara makubwa  kama vile matatizo ya moyo, kushindwa kwa figo, kupata kiharusi, upofu, au uharibifu wa mishipa ya fahamu. 

Hata hivyo, wataalamu wanasema kuwa hali hizi si lazima ziwe hukumu ya kifo. Kupitia utambuzi wa mapema na mabadiliko ya mtindo wa maisha, magonjwa haya mawili yanaweza kudhibitiwa na uhai wa watu ukaokolewa.

‘’Shinikizo la damu linaitwa ‘silent killer’ (muuaji wa kimya) kwa sababu huzioni kabisa dalili na ndiyo maana kwa sasa tatizo hili linaathiri mtu mmoja kati ya watu wazima watatu duniani na kati ya watu watano wenye shinikizo la juu la damu ni mmoja pekee anayeweza kudhibiti hali hiyo kwa matibabu,” anasema Dk Tasekeen Khan, Ofisa wa kitengo cha magonjwa ya moyo na mishipa wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Kuhusu kisukari, mtaalamu wa magonjwa yasiyoambukiza, Dk Omary Ubuguyu anasema:  ‘’ Watu wengi wanachelewa kwenda kupima kisukari, kwani si rahisi kutambua dalili zake ndani ya miaka mitatu mpaka  mitano, utakuta mtu ameshaanza kuathirika viungo kama macho, figo na ubongo,’’ anaeleza.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), zaidi ya watu bilioni 1.3 duniani wanaishi na shinikizo la damu. Kisukari pia kinatoa picha ya kutisha: Shirikisho la Kisukari Duniani (IDF) mwaka 2024  lilikadiria kuwa watu wazima milioni 589  wanaishi na kisukari.

Katika nchi nyingi, mzigo ni mkubwa zaidi katika maeneo ya kipato cha chini na cha kati ambapo mifumo ya afya imeelemewa na uelewa ni mdogo.

Katika nchi za   kusini mwa Jangwa la Sahara, kwa mfano, hadi asilimia 70 ya watu wenye shinikizo la damu hawajagundulika, huku katika baadhi ya maeneo ya Asia, viwango vya kisukari vinaongezeka kwa kasi miongoni mwa watu wazima na vijana kutokana na maisha ya mijini, lishe duni na kutokufanya mazoezi.

“Watu wengi hawatambui kuwa wako katika hatari. Wagonjwa wangu wengi huja hospitalini baada ya kupata matatizo ya maumivu ya kifua, matatizo ya figo, au matatizo ya kuona. Wakati huo, ugonjwa tayari umesababisha madhara makubwa.”  anaeleza mtaalamu mmoja wa afya.

Wengi hatujui tunavyokula

Nje ya lishe duni, kutofanya mazoezi, aina nyingine ya mtindo wa ovyo wa maisha kwa walio wengi ni kutojali kusoma taarifa za onyo kuhusu viambata vya vyakula zinazowekwa kwenye sehemu ya mbele ya vifungashio maarufu Kiingereza kama Front of Pack Labelling- FOPL).

FOPL ni mfumo wa kuweka alama au taarifa muhimu za lishe kwenye sehemu ya mbele ya kifungashio cha chakula mfano, boksi, pakiti, chupa.

 Lengo lake ni kumrahisishia mlaji kufanya uamuzi wa haraka na sahihi kuhusu ubora wa chakula anachonunua na kula. 

Taarifa hii ya lishe inayoonyesha viambata vilivyomo kwenye chakula inapaswa kuwa fupi na iwekwe kwa namna rahisi kueleweka, mara nyingi kwa kutumia alama za rangi, alama za nyota, au nembo maalum.

Magonjwa yasiyoambukiza yanachochewa zaidi na ulaji usiofaa wa vyakula vyenye mafuta mengi, chumvi nyingi, sukari kupita kiasi na nishati nyingi. 

Taarifa hizi zina uhusiano wa karibu na magonjwa haya kwa kuwa huonya mlaji endapo chakula kimejaa sukari, chumvi au mafuta, ambavyo ni vihatarishi vikuu vya magonjwa haya.

Ni taarifa zinazomsaidia mnunuzi. Kwa mfano, mtu akiwa dukani anaweza kuchagua soda yenye sukari kidogo au siagi yenye mafuta kidogo kwa kuangalia alama za mbele ya pakiti.

Kubwa zaidi kadri watu wanavyozidi kuelewa alama hizi, ndivyo jamii inavyopunguza ununuzi wa vyakula visivyo na afya na hivyo kupunguza mzigo wa magonjwa ya kuambukiza.

Madhara kutogundua mapema  magonjwa haya

Madhara ya kugundua magonjwa haya kwa kuchelewa ni makubwa, siyo tu kwa mtu binafsi bali pia kwa familia na mifumo ya afya.

Chukua mfano wa mtu  aliyepuuza  hali yaa kupata uchovu wa mara kwa mara au kupatwa na kiu kingi kwa miaka nenda rudi. Alipoamua kutafuta msaada wa kitabibu, sukari yake ilikuwa juu sana na madaktari walimwambia ana kisukari cha aina ya pili. Ndani ya miezi michache, mtu huyu anapata  uharibifu wa mishipa kwenye miguu yake, hali inayomlazimisha kukosa kazi na kutegemea matibabu ambayo ni  ghali. Huu ndio mfano halisi unaowakumba watu wengi mijini na vijijini.

Maneno kama “Ninatamani ningejua mapema. Kipimo rahisi kingenipunguzia mateso haya yote,” huja kama maneno ya mtu aliyekata tamaa. Kuna msemo usemao’ Majuto ni mjukuu.’’

Ni magonjwa yanayozuilika

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya,  kisukari na shinikizo la damu kwa kiasi kikubwa vinaweza kuzuilika au angalau kudhibitiwa iwapo vitagunduliwa mapema. Msingi ni uchunguzi wa mara kwa mara wa afya.

Shinikizo la damu linaweza kupimwa chini ya dakika moja, huku kipimo rahisi cha damu kikibainisha iwapo mtu ana hali ya kisukari au kisukari kamili  hata kabla dalili hazijaonekana. Lakini watu wengi huepuka vipimo, ama kwa sababu ya gharama, ukosefu wa huduma, au imani ya uongo kuwa kwa sababu wana afya njema, basi hawana hatari za kiafya.

Daktari mshauri mwandamizi magonjwa ya ndani na maradhi ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa Harun Nyagori,  anasema kuna umuhimu kwa jamii kuchunguza afya kwani wengi wenye shinikizo la damu hawafahamu hali zao mapema.

“Tatizo la shinikizo la damu linaweza kukupata na isionyeshe dalili yoyote kwa walio wengi, tatizo ni kubwa kwa kuwa wengi hawatambui hali zao, wanapogundulika tayari madhara ni makubwa mfano tayari ana kisukari, mshtuko wa moyo na matatizo ya figo kushindwa kufanya kazi,” anasema alipozungumza na Mwananchi.

Mabadiliko ya mitindo ya maisha

Wataalamu wa lishe wanapendekeza ulaji wa chakula chenye mizani, kilichojaa mbogamboga, matunda, nafaka kamili, protini zisizo na mafuta mengi, na mafuta yenye afya, huku wakitaka watu kupunguza vyakula vilivyosindikwa, chumvi nyingi na vinywaji vyenye sukari.

Aidha, kutembea kwa dakika 30 kila siku kunaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa hatari ya kupata shinikizo la damu na kisukari. Usimamizi wa msongo wa mawazo, usingizi wa kutosha, na kuepuka tumbaku na pombe kupita kiasi pia ni muhimu.

Kwa waliokwisha gundulika, dawa na udhibiti wa maisha vinaweza kuweka hali zao chini ya usimamizi mzuri wa magonjwa hayo.

Lakini mara nyingi changamoto huwa ni kufuata matibabu kwa muda mrefu. Wengi huacha kutumia dawa pindi wanapojisikia vizuri, bila kujua kwamba magonjwa haya yanahitaji udhibiti wa maisha yote.

Wauaji kimya pia ni tishio kubwa kiuchumi. Matibabu ya madhara yanayotokana na kisukari na shinikizo la damu visivyodhibitiwa kama vile kusafisha damu kwa kushindwa kwa figo, upasuaji wa moyo, au urekebishaji baada ya kiharusi, hugharimu zaidi na pengine watu kufikia hatua ya kufilisika.

Kwa sasa  ripoti zinaonyesha dunia inatumia karibu Dola za Marekani trilioni mbili kwa ajili ya kupambana na magonjwa haya kwa mwaka.  Na huenda kiasi kikafikia trilioni 30 ndani ya miongo miwili ijayo.

Kisukari na shinikizo la damu huenda ni wauaji kimya, lakini si lazima viwe hukumu ya kifo. Siri ipo katika uelewa, kinga, na utambuzi wa mapema.

Kwa mtu binafsi, hii inamaanisha kufanya uamuzi bora wa kiafya na kufanyiwa uchunguzi mara kwa mara. Kwa serikali na mashirika, inamaanisha kuwekeza katika kampeni za uhamasishaji, huduma nafuu za afya, na programu za kijamii.

Ama kwa jamii kwa jumla, lazima kila mmoja avunje  ukimya kuhusu magonjwa haya na kuhamasisha mazungumzo ya wazi kuhusu afya zetu.