Kipa Yanga atimkia Mwanza | Mwanaspoti

KLABU ya Alliance Girls inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake (WPL), imedaiwa ipo katika hatua za mwisho kukamilisha usajili wa kipa wa zamani wa Yanga Princess, Husna Mtunda.

Kipa huyo aliitumikia Yanga Princess kwa misimu miwili, lakini hakupata nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza mbele ya makipa Mghana Safiatu Salifu na Mnigeria Rita Akarekor kwa sasa inaelezwa ameamua kujiongeza kwa kuibukia Alliance yenye maskani yake jijini Mwanza.

Akizungumza na Mwanaspoti, mmoja ya viongozi wa Alliance Girls (jina tunalo) alisema wamekamilisha taratibu zote za usajili isipokuwa bado kumuingiza katika mfumo wa usajili.

“Yupo kambini na wenzake, bado baadhi ya vitu vichache tu hatujakamilisha lakini nafikiri mambo yatakuwa sawa na tutakuwa nae msimu ujao, ni golikipa mzuri,” alisema kiongozi huyo na kuongeza

“Tumejipanga msimu huu, ligi ya msimu uliopita ilikuwa ngumu sana tunajaribu kuongeza maingizo ambayo yana uzoefu mkubwa, tukiwachanganya na wale wa akademi na tuliowapandisha italeta ushindani kidogo.”

Iko hivi. Ligi ya wanawake huchelewa kuanza inategemea na ratiba ya michuano ya kimataifa ambayo bingwa ligi JKT Queens anawakilisha michuano ya Ligi ya Mabingwa hivyo hadi dirisha dogo la usajili timu ambazo hazikukamilisha taratibu za usajili zinawaingiza tena kwenye mfumo.

Hivyo asilimia kubwa ya wachezaji wamesaini mikataba ya timu na wako kambini lakini bado hawajaingiza katika mifumo inayotambulika na Shirikisho la Soka nchini (TFF).