Dar es Salaam. Mara nyingi kupiga mluzi huchukuliwa kama ishara ya mtu kuchoka, kutojali au hata burudani ya muda.
Hata hivyo, wataalamu wa afya wanasema tendo hili lina faida nyingi kwa mwili wa binadamu, hususani katika kuboresha mfumo wa upumuaji, kuimarisha mzunguko wa damu na kuongeza ustawi wa akili.
Kwa mujibu wa wataalamu, kupiga mluzi ni njia ya asili ya mwili kujipumzisha, kurejesha usawa wa hewa na kuongeza oksijeni kwenye damu.
Mtu anapopiga mluzi, mapafu hupanuka zaidi na mishipa ya damu katika ubongo hupokea hewa safi kwa wingi. Hali hii husaidia kupunguza uchovu, kuongeza umakini na kupunguza msongo wa mawazo.
Utafiti umeonyesha kuwa kupiga mluzi pia huamsha misuli ya uso na koo, jambo linalosaidia kulainisha mishipa ya sauti na kudhibiti mapigo ya moyo.
Daktari mstaafu wa masuala ya mfumo wa damu, Dk Neema Omari, anasema kupiga mluzi ni zoezi muhimu kwa afya ambalo watu wengi bado hawalijui.
“Kupiga mluzi husaidia kuongeza urefu wa nyuzi za misuli, kuboresha mzunguko wa damu na kuongeza uwezo wa viungo kustahimili mifadhaiko ya kimwili ya kila siku,” anasema.
Anaongeza kuwa watu wanaopiga mluzi mara kwa mara huwa katika nafasi ndogo ya kupata majeraha ya misuli au viungo, hasa wanapofanya kazi au mazoezi ya nguvu.
Aidha, mluzi anasema husaidia kuboresha mkao wa mwili, kupunguza maumivu ya mgongo wa chini na kuongeza ufanisi wa viungo.
Kwa upande wake, Dk Ismail Omary, mtaalamu wa upumuaji, anasema kupiga mluzi ni muhimu zaidi kwa watu waliopata upasuaji wa mapafu kwa sababu huashiria kurejea kwa afya ya mfumo wa upumuaji.
“Mtu anapopiga mluzi, anajifunza uwezo wa mapafu katika kuingiza na kutoa hewa. Ni njia rahisi na ya asili ya kuimarisha misuli ya upumuaji,” anaeleza.
Anawashauri watu wenye matatizo ya kupumua, wapige mluzi au wapulize puto na filimbi mara kwa mara kama mazoezi ya kuimarisha mapafu yao.
Naye Dk Daud Kipenda, bingwa wa masuala ya misuli na mifupa, anasema kupiga mluzi, huchochea misuli ya mikono na miguu, huongeza mzunguko wa damu na kusaidia mfumo wa neva kufanya kazi kwa ufanisi.
“Kwa mtu anayefanya kazi za ofisini au anayekaa muda mrefu, kupiga mluzi husaidia kupunguza msongamano wa misuli na kuingiza oksijeni zaidi kwenye viungo vya mwili,” anafafanua na kuongeza:
“Kazi za kitafiti zinaonyesha kupiga mluzi huchochea uzalishaji wa homoni za furaha kama serotonin na endorphins, ambazo hupunguza msongo wa mawazo na kuongeza ustawi wa akili.”
Mtaalamu wa saikolojia, Modesta Kimonga, anasema kupiga mluzi ni matokeo ya mihemko ya mwili na akili yanayolenga kupunguza shinikizo la kihisia.
“Mwili wa binadamu umeumbwa kupitia hisia mbalimbali. Kupiga mluzi ni mojawapo ya matokeo ya kihisia ambayo huashiria mwili umefurahishwa au unahitaji kitu fulani,” anasema.
Naye John Richard, mtaalamu wa saikolojia ya mwili na akili, anaeleza kuwa kupiga mluzi huchochea mfumo wa neva uitwao ‘parasympathetic’, unaohusika na hali ya utulivu.
Husaidia kupunguza homoni ya msongo wa mawazo na hivyo kuongeza utambuzi wa mwili pamoja na umakini wa akili.
Anapendekeza watu wanaokabiliwa na msongo wa mawazo, wasiwasi sugu au hata unyogovu wa muda mrefu, wajumuishe mluzi katika ratiba zao za kila siku ili kudhibiti hali zao za kihisia.
Mkazi wa Mabibo, Dar es Salaam, Shafii Sanga, anasema hakuwahi kufahamu kuwa kupiga mluzi kuna faida kiafya, kwani yeye hufanya hivyo tu kwa burudani wakati wa kazi zake ndogo ndogo.
“Mimi hupiga mluzi kwa ajili ya burudani au kumuita mtu. Sijawahi kusikia kama kupiga mluzi kuna faida yoyote kwa mwili wa binadamu, lakini sasa najua kuwa ni jambo la msingi kiafya, hivyo utakuwa utamaduni wangu wa kila siku,” anasema.
Kwa upande wake, Asha Said, mfanyabiashara wa matunda katika soko la Tandika, anasema huwa anapiga mluzi akiwa kazini, jambo ambalo mara nyingine humfanya wateja wake wake wamshangae.
“Nikiwa kazini napiga mluzi kwa ajili ya kufurahisha. Wanaume huwa wananikataza wakisema ‘mwanamke mzima unampiga mluzi kama mwanaume’, lakini sikuwahi kujua kuwa kuna faida ya kiafya. Kuanzia sasa nitahamasisha hadi familia yangu tufanye hivyo kila siku,” anaeleza.
Kwa mujibu wa Dk Christian Agudelo, mtafiti wa masuala ya neva kutoka Chuo Kikuu cha Miami, kupiga mluzi ni mwitikio wa kiasili unaotokea kabla ya mwili kuhamia kutoka hali ya chini ya utendaji kwenda hali ya juu ya utendaji. Ni ishara kwamba mwili unajiandaa kufanya kazi kwa umakini zaidi.
Katika jarida la Harvard Men’s Health Watch, Mhariri Mtendaji, Matthew Solan anaeleza kuwa kupiga mluzi huongeza mapigo ya moyo, kupanua misuli na kuandaa mwili kuwa makini zaidi baada ya kupumzika.
Utafiti wa Andrew C. Gallup, mhadhiri wa saikolojia, unaonyesha kuwa mluzi husaidia kupunguza joto la ubongo kwa kuruhusu hewa baridi kuingia, hivyo kuimarisha uwezo wa kufikiri.
Ingawa kwa wengi kupiga mluzi huonekana kama burudani au tabia ya kawaida, wataalamu wa afya wanasisitiza ni mojawapo ya mazoezi ya asili yenye faida lukuki kiafya na kisaikolojia.
Ni ishara ya mwili kujiandaa, kujikinga na kujirekebisha. Kwa hiyo, usipuuze mluzi wako kwani unaweza kuwa tiba unayoikosa.