Dar es Salaam. Baada ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kumuita aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole kutoa maelezo na ushahidi wa tuhuma alizoibua mtandaoni, yeye amesema ipo nia njema na ovu kwenye wito huo.
Kwa mujibu wa Polepole, ipo dhamira njema na ya dhati kwenye wito wa polisi wa yeye kuhitajika kutoa maelezo na ushahidi na upande wa pili, ipo nia ovu kwenye wito huo, hivyo akahoji kwa nini wasimhoji kwa njia ya mtandao.
“Kuna watu wanataka niende pale Polisi ukifika pale unakamatwa, kwa sababu hakuna sehemu wamesema kuna tuhuma kwangu, unaweza ukaachiwa halafu baadaye unapotea na Polisi hawahusiki,” amesema Polepole jana Septemba 18, 2025 alipozungumza kwa njia ya mtandao akijibu wito wa polisi.
Polepole alijiuzulu ubalozi nchini Cuba, Julai 13, 2025 kwa madai hawezi kuendelea kuwa sehemu ya uongozi usiohamasika na utii wa misingi ya Katiba ya nchi na chama, haki, maadili, utu na uwajibikaji kwa wananchi.
Tangu wakati huo, amekuwa akiibua tuhuma mbalimbali dhidi ya Serikali, taasisi zake na baadhi ya watu binafsi.
Agosti 5, 2025, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kupitia kwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Balozi Samwel Shelukindo ilieleza kupokea barua kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka ikitaarifu kuwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa mamlaka aliyo nayo chini ya Katiba ya Tanzania, ametengua uteuzi wa Polepole na kumuondolea hadhi ya ubalozi.
Septemba 15, 2025 Misime alisema Jeshi la Polisi limefungua jalada la uchunguzi na linaendelea kuchunguza tuhuma zilizotolewa na Polepole.
“Tuhuma ambazo ametoa na anaendelea kuzitoa kulingana na jinsi alivyozielezea zinaashiria uwepo wa makosa ya kijinai na kwa mujibu wa sheria zinahitaji ushahidi wa kuzithibitisha zitakapowasilishwa mahakamani,” ilieleza taarifa ya Polisi na kuongeza:
“Tuhuma hizo amekuwa akizitoa kupitia mitandao ya kijamii, baada ya kufungua jalada na kuanza uchunguzi, Jeshi la Polisi mbali na kukusanya ushahidi, limekuwa likifanya jitihada za kumpata ili aweze kutoa maelezo au ushahidi na vielelezo vitakavyothibitisha tuhuma hizo ili kuwezesha hatua zingine za kisheria ziweze kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria na ndivyo utaratibu wa kisheria ulivyo.”
Jeshi hilo pia limemwelekeza Polepole aliyewahi kuwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), kufika ofisi ya DCI kutoa maelezo yake au ushahidi kuhusu tuhuma anazotoa kwa umma kupitia mitandao ya kijamii.
Polepole amesema kuitwa kwake ni dalili njema kwamba, Jeshi la Polisi limesikiliza na kuona mahali penye viashiria vya jinai, hivyo kuona vema wamtafute awaongezee maelezo na ushahidi.
“Hili ni jambo jema na huu ni upande mmoja. Unajua wananchi huko mtaani wana mashaka kweli na hii kitu inaniumiza, ni waoga mno, watu wanakutumia ujumbe mtandaoni samahani endelea kusema,” amedai.
Upande wa pili, amedai ni ujanjaujanja akieleza jeshi hilo limemtafuta bila mafanikio, akihoji endapo kuna mtu ndani ya Serikali anayemtaka akamkosa kwa njia ya mawasiliano.
Amesema kama Polisi hawana namba yake na simu, wangewasiliana na Wizara ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Afrika Mashariki na angepatikana kwa kupigiwa simu moja pekee.
“Katibu mkuu na Katibu mkuu wangezungumza wangepata namba zangu, najibu ujumbe mara kadhaa nikiwa mazingira rafiki, napokea simu tunazungumza mara nyingi,” amesema.
Polepole amedai: “Lakini katika upande huohuo mmekuwa mkinitafuta kwa kificho si kwa maana njema, nilipojiuzulu tu kuna watu waliofika nyumbani kwangu Masaki wakazingira nyumba wakiamini nitakuwa ndani na sikuwepo.”
Amedai watu wenye silaha za moto walikwenda kuweka kambi kwa dada yake na kutokomea naye na alipaza sauti juu ya tukio hilo.
Polepole amesema hata kabla ya hapo alikwishavamiwa na nyumbani mara mbili na Jeshi la Polisi lilichukua maelezo lakini hakuna maendeleo ya uchunguzi, hivyo kama linataka kuzungumza naye hadharani basi wazungumze na si kumtafuta kwa kificho.
