Songea. Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) zitahamia mkoani Ruvuma ambako mgombea urais, Samia Suluhu Hassan na mgombea mwenza, Dk Emmanuel Nchimbi watafanya mikutano kwa siku tatu tatu.
Samia na Dk Nchimbi wanakutana tena katika mkoa mmoja tangu walipozindua kampeni za chama hicho kitaifa, Agosti 28, 2025 kwenye Uwanja wa Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam.
Baada ya uzinduzi, wagombea hao waligawana maeneo kwenda kueleza kile walichokifanya miaka mitano iliyopita na wanachotarajia kukifanya endapo watachaguliwa tena.
Katika mikutano yao, sekta ya elimu, afya, maji, miundombinu ya barabara na madaraja, ruzuku ya mbolea na mbegu, kilimo, ufugaji na kukuza utalii ni miongoni mwa maeneo ambayo wanayaeleza kwa kina.
Dk Nchimbi atawasili leo Ijumaa, Septemba 19, 2025 katika Uwanja wa Ndege wa Songea akitokea Dar es Salaam alikokwenda kwa mapumziko. Rais Samia atawasili kesho Jumamosi.
Baada ya uzinduzi, Samia alianzia Morogoro, Dodoma, Songwe, Mbeya, Njombe, Iringa, Singida, Tabora, Kigoma na mikoa mitatu kati ya mitano ya Zanzibar ambayo ni Kusini Unguja, Kaskazini Unguja na Kusini Pemba.
Dk Nchimbi yeye alianza mikoa ya Mwanza, Mara, Simiyu, Shinyanga, Geita, Kagera, Rukwa, Katavi, Arusha, Kilimanjaro, Tanga na sasa yuko Ruvuma.
Mpaka sasa, Samia amefanya kampeni kwenye mikoa 13 na Dk Nchimbi mikoa 11, jumla inakuwa mikoa 24 kati ya 31 ya Tanzania, kwenye siku 30 za kwanza za kampeni kati ya 61.
Kwa mujibu wa ratiba ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Dk Nchimbi atakuwa na siku tatu, kuanzia Septemba 20 hadi 22, huku mgombea urais Samia atakuwa Ruvuma kuanzia Jumapili ya Septemba 21 hadi 23, 2025.
Baada ya mkutano wa Ruvuma, Samia atakwenda mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani huku Dk Nchimbi akipita Njombe na Iringa.
Viongozi hao kukutana mkoani humo kumeufanya mkoa kuwa na pilikapilika za hapa na pale, huku huduma za malazi hazipatikani kiurahisi.
Kuna watu watalazimika kwenda kulala maeneo ya jirani kama Namtumbo, Mbinga au Mbambabay, ambapo ni zaidi ya kilomita 60 hadi 100 kutoka Songea.
Wasafirishaji mathalani wa bodaboda wanachekelea kutokana na ugeni huo, hasa wanapohitajika kutoka eneo moja kwenda jingine. Wauzaji wa vyakula na wote wanaohusika na biashara mbalimbali ni fursa pia.
Mwananchi limezungumza na baadhi ya wananchi mkoani humo kupata matarajio yao ya Samia na Dk Nchimbi kufika mkoani humo kunadi sera zao.
John Haule, mkazi wa Ndilimalitembo Songea, anasema anatumaini ujio wa Rais Samia utasaidia kuongeza bei ya mahindi kutoka Sh700 kwa kilo moja ambayo sasa imedumu kwa zaidi ya miaka mingi na kufikia Sh1,000 kwa kilo.
Anasema pamoja na wakulima kulima kwa bidii bado pembejeo za kilimo zipo juu, ikiwemo mbegu na mbolea pamoja na viuatilifu, hivyo Serikali isaidie kupunguza bei ya pembejeo ili kumrahisishia mkulima kumudu gharama hizo.
“Wakulima wengi wana mahindi, ila wameshindwa kuuza kwani bei ipo chini na ukumbuke mwaka huu wa kulima wengi wamepata hasara kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi,” anasema Haule akisisitiza anatamani kusikia wanasaidiwaje juu ya bei.
Naye Aidan Ngonyani anasema atafurahi iwapo Serikali italipa madeni ya wazabuni mbalimbali kwa wakati maana wengi wanadai na wamekata tamaa kutokana na kutolipwa kwa wakati.
“…sikufichi, maisha ya wazabuni wengi yanakatisha tamaa. Wengi wana madeni makubwa benki na baadhi wamekata tamaa, wanaidai Serikali na haijawalipa kwa wakati. Wengine wameuza mali zao na kusababisha familia kusambaratika.
“Serikali iangalie kwa jicho la huruma, maisha ni magumu sana mtaani kadri siku zinavyosonga hali inazidi kuwa mbaya,” anasema Ngonyani.
Kwa upande wake, mjasiliamali wa Manispaa ya Songea, Seky Erenest, anasema anatamani ujio wa viongozi hao uwasaidie wajasiliamali wadogo walioomba mikopo ya asilimia kumi wapatiwe bila usumbufu au upendeleo.
“Mikopo inatolewa kwa upendeleo, inachukua muda mrefu na wengine hatupatiwi kabisa wakati tuna vigezo vyote. Hivyo tunaomba uwekwe utaratibu mzuri utakaotusaidia wote kupata mikopo,” anasema Seky.
Sauda Hashim, mkazi wa Bombambili Manispaa ya Songea, anatamani Dk Nchimbi awasaidie kurudisha vyuo vikuu vilivyofungiwa Songea ili watoto wanaotoka familia maskini waweze kupata elimu wakiwa karibu na mazingira ya nyumbani.
Agnes Komba, mkazi wa Mahenge, anaomba Samia awasaidie wanawake wa Mkoa wa Ruvuma mikopo ya kilimo ili wazalishe kwa wingi chakula na baadaye waweze kuuza ndani na nje ya nchi, hivyo kujiongezea kipato.
Endelea kufuatilia Mwananchi kujua yanayotokea kwenye mikutano hiyo…