:::::::::
Mkuu wa Wilaya ya Ilala amepokea rasmi vifaa vya kazi, mavazi ya kujikinga kwa wahudumu wa afya, pamoja na magari mawili na baisikeli 56 kutoka kwa Shirika la UNFPA na AMREF kwa kushirikiana na serikali ya Canada kupitia Global Affairs.
Vifaa hivi vimekabidhiwa kwa ajili ya kuunga mkono jitihada za Serikali za kupunguza vifo vya mama na watoto wachanga nchini, chini ya mwongozo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza wakati wa zoezi la makabidhiano, Balozi wa Canada nchini Tanzania, Emily Burns, alisema serikali yao inajivunia ushirikiano huu wa dhati na Tanzania katika kuboresha huduma za afya.
“Kuwekeza katika wakunga na wahudumu wa afya ni kuwekeza katika utu, usawa wa kijamii na mustakabali wa familia za Kitanzania,” alisema Balozi Burns.
Aidha, alisema magari mawili yaliyotolewa yataongeza ufanisi wa usimamizi na uratibu wa huduma za uhamasishaji ili kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi wote.
Mradi huu unalenga kusaidia kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu (SDG 3) na Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050 kwa kuimarisha huduma za afya kuanzia ngazi ya jamii.