Iringa. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Jimbo la Iringa Mjini, Frank Nyalusi amefariki dunia usiku wa kuamkia leo, Septemba 19, 2025.
Nyalusi ambaye amewahi kuwa diwani Kata ya Mivinjeni, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa (2010 – 2020), amefariki duinia akipatiwa matibabu kwenye chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu (ICU), kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo, Septemba 19, 2025 Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Taifa (Bavicha) kupitia Chadema, Necto Kitiga amesema msiba upo nyumbani kwa marehemu katika Mtaa wa Mawelewele, huku mazishi yakitarajiwa kufanyika kesho.
Kitiga amesema kifo cha Nyalusi ni pigo kubwa kwa chama, akibainisha kuwa baadhi ya viongozi wa juu wa Chadema Taifa wanatarajiwa kufika Iringa kushiriki mazishi hayo.
“Amekuwa kiongozi aliyeheshimika sana kwa msimamo wake na uzalendo, tutamkumbuka kwa mchango wake mkubwa katika kuimarisha chama Iringa,” amesema Kitiga.
Endelea kufuatilia mitandao ya Mwananchi Digital kwa taarifa zaidi za msiba huu.