Dodoma. Wazazi wametajwa kuwa chanzo cha ukatili kwa watoto wao na mara nyingi kushindwa kupata taarifa sahihi za matendo wanayotendewa watoto katika jamii.
Kauli hiyo imetolewa jana Alhamisi, Septemba 17, 2025 jijini Dodoma na Naomi Maswaga kwenye mkutano wa pili wa mwaka wa jukwaa la Msichana Café unaodhaminiwa na shirika lisilo la kiserikali la Msichana Initiative.
Naomi (64), mmoja wa wasimamizi na watoa elimu kwa jamii, amesema kauli za makemeo ya wazazi kwa watoto wao hasa wa kike zimekuwa mwiba na maumivu kwa mabinti.

Mkurugenzi wa taasisi ya Msichana Initiative, Consolata Chikoto.
Amesema mtoto anayekemewa zaidi na mzazi wake hawezi kuwa huru na kueleza mambo mengi anayokutana nayo kwa jamii hata shuleni.
“Watoto wanakosa uhuru, wananyanyasika, hawana mtu wa kuwapokea makovu yao kwani wazazi hawawapi nafasi ya kuzungumza nao, badala yake wanakuwa wakilia kila wakati wanapoguswa. Je, mtoto atasema nini?” amesema Naomi.
Kwa mujibu wa mama huyo, Msichana Initiative imekuwa na kazi kubwa ya kutoa elimu shuleni na kwenye jamii ili watu wabadili mitazamo yao, na tayari wamefanikiwa kuwarudisha shuleni wanafunzi waliokatisha masomo yao kwa sababu ya mimba.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Msichana Initiative, Consolata Chikoto, amesema kazi kubwa inayofanyika hivi sasa ni kupeleka elimu kwa jamii, wanayoifanya katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Pwani na Tabora, na imezaa matunda kwa kiasi kikubwa.

Baadhi ya wanachama wa taasisi ya Msichana Initiative kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania.
Chikoto amesema wanatumia mbinu mbalimbali ili kubaini matatizo yanayowakabili wasichana na kuwapatia suluhisho la kuwafanikisha kuzifikia ndoto zao hasa kwenye mipango ya elimu.
Hata hivyo, amekiri bado kuna changamoto kwenye suala la ndoa za utotoni, kazi aliyosema vikundi vya watu waliofundishwa ndivyo vinavyofanya kazi kubwa kwa kushirikiana na Serikali ngazi za chini.
“Jukumu letu kubwa ni ulinzi na utetezi kwa watoto wetu. Kupitia hawa wanavikundi tumeanza kupata mafanikio kwa kiasi kikubwa katika suala la kuwarudisha shuleni watoto wa kike, lakini ndoa za utotoni nazo zinaanza kupungua kwa kiasi. Yote yanafanywa na wanavikundi hawa,” amesema Chikoto.
Kwa upande wake, Ramadhan Mihambo amesema maeneo ya vijijini bado kuna ukatili huku suala la mila potofu likiwa limechukua nafasi kubwa.
Mihambo, anayetoka Wilaya ya Nzega, mkoani Tabora, ameeleza kuwa katika maeneo ya vijijini tatizo la ndoa za utotoni bado linachukua nafasi.