Zitto, Baba Levo wasaka rekodi Kigoma Mjini

Kigoma. Jimbo la Kigoma Mjini ni miongoni mwa majimbo yanayoibua mjadala na kufuatiliwa na wengi kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025.

Siku hiyo Watanzania wataamua nani atakayeshika hatamu za urais, ubunge na udiwani kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Macho mengi yanaitazama Kigoma Mjini, ambayo pia imekuwa midomoni mwa watu ambako historia, siasa na burudani vimekutana ana kwa ana.

Kwenye kona moja ya ulingo wa kisiasa amesimama Zitto Kabwe, mwanasiasa mkongwe anayejulikana kwa misimamo yake na historia ndefu bungeni.

Zitto ni mgombea wa ACT-Wazalendo, anayejaribu kurejea jimboni alikopata umaarufu kwa muda mrefu.

Mwaka 2005, kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), aliingia katika ulingo wa siasa, akang’ara kwa kumshinda mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Halimenshi Mayonga, akaongoza Jimbo la Kigoma Kaskazini kwa vipindi viwili mfululizo.

Safari yake ikamfikisha kwenye nafasi nyeti bungeni kama Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na baadaye Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC).

Akiwa Chadema, Zitto alishika wadhifa wa Naibu Katibu Mkuu (Bara) kwa miaka saba hadi alipohama chama hicho na kujiunga na ACT-Wazalendo, ambako alichaguliwa kuwa Kiongozi wa Chama (KC) kuanzia 2015 hadi 2025 alipostaafu uongozi.

Kwenye Uchaguzi Mkuu 2020 alishindwa kutetea kiti cha ubunge baada ya kuangushwa na mgombea wa CCM, Kilumbe Ng’enda.

Kona ya pili ya ulingo huo katika uchaguzi wa mwaka huu, yupo mpinzani wa kipekee, msanii wa muziki wa kizazi kipya, Clayton Chipando maarufu Baba Levo.

Mwanamuziki huyu, aliyewahi kuwa diwani wa Mwanga Kaskazini katika Halmashauri ya Manispaa Kigoma Ujiji kuanzia mwaka 2015 hadi 2020 kupitia ACT-Wazalendo, amehamia CCM na amepania kurudi katika siasa akiwania ubunge.

Katika Uchaguzi Mkuu 2020 Baba Levo aligombea udiwani kwenye kata hiyo lakini alishindwa na mgombea wa CCM, Sharon Mashanya. Tangu wakati huo alipumzika shughuli za kisiasa hadi alipotangaza kujiunga na CCM mwaka 2025.

Historia ya wawili hawa ina mvuto wa kipekee, wote wamezaliwa na kukulia Mwanga Kaskazini, Barabara ya Kisangani. Kwa wakati mmoja walihudumu katika uongozi kupitia chama kimoja, ACT-Wazalendo, Zitto akiwa mbunge na Baba Levo kwa nafasi ya udiwani.

Ushindani kati yao umechochea gumzo mitaani. Kwa mujibu wa watu wanaofuatilia mwenendo wa kampeni za uchaguzi huo zilizoanza Agosti 28, 2025, Baba Levo anaungwa mkono zaidi na vijana na kinamama, akikubalika kama sauti ya kizazi kipya.

Zitto, kwa upande mwingine, anakubalika na mtandao wa wasomi, wapigakura wazoefu na kwa historia zake alipokuwa mbunge.

Wawili hao wameshazindua kampeni zao, wakiendelea kusaka kuungwa mkono wakinadi sera kupitia ilani za uchaguzi za vyama vyao.

Ahadi kwa wananchi pia zinaonesha tofauti ya falsafa zao. Baba Levo anajikita kwenye kuboresha huduma za kila siku za wananchi kwa maana ya barabara za mitaa kuwa za kiwango cha lami, masoko ya jioni yakiwemo ya Marungu, Noti na Gungu kuwa na mwonekano wa kisasa, kufunga taa, kugawa meza mpya kwa wajasiriamali na hata Wi-Fi ya bure sokoni.

Ameahidi kuhakikisha kila mwanafunzi anapata dawati, kusimamia wakandarasi wanaojenga miradi ya Soko la Mwanga, kutoa maji katika Bwawa la Katubuka, ujenzi wa Uwanja wa Ndege Kigoma na barabara ya Bangwe hadi Ujiji ili ikamilike kwa wakati.

Kwa kauli yake amesema: “Mkinichagua nitajenga soko jipya katika Kata ya Kibirizi baada ya lililopo kujaa maji ya Ziwa Tanganyika. Nitatetea watu watakaokuwa wanasumbuliwa na Idara ya Uhamiaji kwa kigezo cha kutokuwa raia wa Tanzania, nitatetea waendesha bajaji na bodaboda wanapoonewa au kusumbuliwa na askari wa usalama barabarani.”

Zitto, kwa lugha ya uzoefu, ameeleza dhamira ya kuendeleza alipoishia. Anazungumzia ajira za vijana kupitia sekta mbalimbali, miradi mikubwa ya kiuchumi kama bandari, reli na viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya ziwani

Akizindua kampeni, Zitto amewaomba wananchi wamchague akaendeleze alipoishia mwaka 2020 kwa kukamilisha miradi yote iliyokwama.

Pia, ameahidi kuwezesha uchumi unaozalisha ajira kwa vijana kwa sekta zote, kukamilisha miradi ya ujenzi wa daraja la Mto Luiche, kilimo cha umwagiliaji katika bonde la mto huo na miradi aliyoianza wakati wa kipindi chake cha ubunge.

“Wakati wa kipindi changu nilikuwa natetea watu wanaosumbuliwa na Idara ya Uhamiaji kuhusu uraia wao. Nilianza kuifanya Kigoma kuwa kituo cha biashara na lango la Maziwa Makuu kwa kuimarisha bandari, Jiji la Ujiji, usafiri wa maji na reli, viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya ziwani, masoko ya biashara za kimataifa. Hivyo, mkinipa ridhaa yenu naenda kukamilisha miradi hiyo yote,” alisema.

Zitto amesema atarejesha miradi kabambe ya barabara za mitaa, barabara ya Kasulu, mifereji ya maji ya mvua, kurejesha mpango wa bima ya afya kwa wote kupitia mfumo wa hifadhi ya jamii, kuboresha elimu ya msingi na sekondari na kusukuma ajenda ya kuanzishwa kwa chuo cha ufundi mchundo na chuo kikuu cha Kigoma.

Kwa Zitto, ni kama amesema: “Mlinipa nafasi, nilianza; sasa nirudisheni nikamilishe.”

Taswira ya yanayoendelea inaibua kitendawili. Je, wapigakura watamchagua msanii na mwanasiasa anayeahidi kuboresha maisha ya kila siku au mwanasiasa mzoefu mwenye kumbukumbu ya miradi mikubwa ya maendeleo?

Ushindani na mnyukano dhidi ya wawili hao ulidhihirika hata wakati wa kampeni za urais za mgombea wa CCM, Samia Suluhu Hassan, alipokuwa Kigoma Mjini, alipoulizwa na Baba Levo ni nani kati ya “watoto wake wawili” anamuunga mkono. Samia alijibu wote ni watoto wake, jibu lililoibua hisia kwa sababu linaakisi taswira ya jamii iliyogawanyika kati ya wagombea hao, mmoja wa CCM na mwingine ACT-Wazalendo.

Nani ataibuka mshindi? Hilo ni swali gumu kujibu kwa sasa kutokana na ushindani uliopo baina ya Zitto na Baba Levo, ambao ushiriki wao kwa pamoja umeleta hamasa ambayo haijawahi kuonekana kwa kipindi kirefu katika uchaguzi kwenye jimbo hilo.

Ni vigumu kutabiri matokeo, lakini jambo moja ni wazi, Oktoba 29, 2025, wapigakura wa Kigoma Mjini watakata mzizi wa fitna. Wataamua hatima ya washindani hao wawili kutoka Barabara ya Kisangani.