Puma yaboresha upatikanaji wa nishati Singida

Dar es Salaam. Kampuni ya Puma Energy imezindua kituo cha huduma mkoani Singida, ikisema hatua hiyo inalenga kuboresha upatikanaji wa nishati, kuunda fursa za kiuchumi na kutoa huduma za kisasa kwa wananchi.

Kituo hicho kipya kimeelezwa kitachangia kukuza maendeleo ya kiuchumi ya mkoa huo na maeneo ya jirani.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kituo hicho, jana, Septemba 18, 2025, Mkuu wa Kitengo cha Biashara Puma Energy Tanzania, Benedict Ndunguru, amesema wamedhamiria kushirikiana na wananchi na kutoa mchango katika ukuaji wa Taifa.

Amesema ujenzi wa kituo hicho ni wa kimkakati wenye lengo la kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya mafuta na huduma nyingine katika eneo hilo.

“Uzinduzi wa kituo hiki ni uthibitisho wa kujitolea kwetu kuwaletea jamii suluhisho za nishati zilizo salama, za kuaminika na za kisasa karibu zaidi na wao,” amesema.

Amesema uwekezaji huo utatoa ajira, kusaidia wasambazaji wa mafuta wa ndani na kuchangia moja kwa moja kwenye ukuaji wa uchumi.

Mkuu wa Kitengo cha Sheria na Masuala ya Uhusiano wa kampuni hiyo, Emmanuel Bakilana, amesema usalama na ubora wa bidhaa ni nguzo kuu ya shughuli za Puma.

“Usalama ndiyo msingi wa kila jambo tunalofanya. Kupitia viwango vyetu vya utendaji na msisitizo wa kutoa mafuta na vilainishi vya ubora wa juu, tunahakikisha wateja wanapata siyo tu nishati ya kuaminika, bali huduma zinazowawezesha kufanikisha malengo yao na kukua,” amesema.

Kituo hicho, mbali na huduma za mafuta, kinatoa zingine za gym, mgahawa, duka, ofisi na za matengenezo na kuosha magari.

Kwa mujibu wa kampuni hiyo, kituo hicho kimejengwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya Puma vya afya, usalama, ulinzi na mazingira (HSSE).