Sababu Mkurugenzi halmashauri kutupwa jela miaka 20

Moshi/Simanjiro. Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Samwel Gunza amehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 20 jela kwa kosa la matumizi mabaya ya madaraka.

Gunza amehukumiwa adhabu hiyo Septemba 18, 2025 na Hakimu Mkuu Mkazi, Charles Uiso wa Mahakama ya Wilaya Simanjiro, ambaye amesema Jamhuri imethibitisha mashtaka dhidi yake pasipo kuacha shaka yoyote.

DED huyo wa zamani alikuwa akikabiliwa na mashtaka mawili yanayoangukia katika Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022 na Sheria ya Uhujumu Uchumi na Makosa ya Kupangwa ya 2022.

Katika kosa la kwanza, ilidaiwa na upande wa mashtaka kuwa kati ya Februari 17 na Machi 30, 2023 katika Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, mshtakiwa alitumia vibaya madaraka yake ya DED wa halmashauri hiyo.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, kwa makusudi, Gunza alitumia vibaya madaraka yake kwa kutoa zabuni ya kukusanya mapato yanayotokana na mazao ya mifugo katika Soko la Orkesumet kwa Elias Tipiliti bila kutangaza zabuni.

Kitendo hicho kilikiuka kifungu cha 67, 68(1), (2), (3), (4) na (5) cha Sheria ya Ununuzi namba 410 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022 na Kanuni iliyotangazwa katika GN namba 446 ya mwaka 2013 na kujipatia faida isiyofaa.

Ilidaiwa pia kuwa katika kipindi hichohicho, wakati akitimiza majukumu yake kama DED, alitoa zabuni ya kukusanya mapato yatokanayo na mifugo katika soko hilo kinyume cha Sheria ya Ununuzi wa Umma na Kanuni namba 446 ya 2013.

Katika shauri hilo la jinai, mshtakiwa alikana kutenda kosa, Jamhuri iliita mashahidi sita, akiwamo mfanyabiashara Tipiliti ambaye ndiye alipewa zabuni.

Tipiliti katika ushahidi alieleza Februari 16, 2023 aliwasilisha kwa Halmashauri ya Simanjiro, maombi ya maandishi akiomba kupewa fursa ya kukusanya mapato katika soko Orkesumet.

Baadaye akapokea barua kutoka kwa mkurugenzi ya uteuzi wa kukusanya ushuru kama alivyoomba. Alidai hakuna Bodi ya Zabuni iliyowahi kumwita kupitisha maombi yake ya kazi hiyo.

Shahidi wa kwanza, Dominica Ngaleka aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Zabuni ya halmashauri hiyo, alieleza Februari 2023 bodi hiyo haikuwahi kukaa kujadili na kutoa mapendekezo kuhusu ukusanyaji mapato katika soko hilo.

Shahidi wa tatu, Edward Casmir, mhasibu wa halmashauri alidai Februari 22, 2023 alimwandikia barua DED (mshtakiwa) akimshauri azingatie mchakato wa kutangaza zabuni hiyo ili kuhakikisha mchakato unafuata sheria ili mzabuni bora ndiye anapewa kazi.

Ofisa ununuzi, alikuwa mkuu wa Idara na Katibu wa Bodi ya Zabuni, Mussa Kimwanga aliyekuwa shahidi wa tano aliyedai mwaka 2022 hadi 2023, halmashauri haikuwahi kutangaza zabuni kuhusu soko hilo.

Mshtakiwa katika utetezi, alidai si zabuni zote hutangazwa na kwamba, kulikuwa na haja ya haraka ya kumtafuta mtu wa kukusanya mapato ya mifugo katika soko hilo.

Alidai hilo hufanyika kwa kumpa mtu ambaye anakuwa ameomba kwa wakati huo.

Alidai Tipiliti, alipoomba kukusanya mapato kwa kumwandikia barua yeye, naye aliipeleka kwa mkuu wa idara ya sheria na ununuzi ili amshauri na wajibu wake uliishia.

Alidai mkuu wa idara ya ununuzi alishauri kutafuta mtu wa nje (outsource) kwa kuwa halmashauri ilikuwa ikipoteza mapato, hivyo alimteua Tipiliti kama chanzo kimoja.

Hakimu Uiso amesema baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili katika shauri hilo, ameona hakuna ubishi kuwa mshtakiwa alikiuka mamlaka yake kwa kumteua mzabuni huyo.

Baada ya kuchambua ushahidi huo, mahakama iliona mshtakiwa alikuwa na hatia katika kosa la kwanza la kutumia vibaya madaraka yake, hivyo amemtia hatiani na kumhukumu kutumikia kifungo cha miaka 20 jela.

Kwa kosa la pili ambalo pia amesema lilithibitishwa pasipo kuacha shaka, amemtia hatiani mshtakiwa na kumhukumu kutumikia kifungo cha cha miaka miwili jela. Hakimu amesema adhabu hizo zitatumikiwa kwa pamoja, hivyo atatumikia jumla miaka 20.