Dar es Salaam. Wafanyabiashara watatu, wakazi wa Manzese, jijini Dar es Salaam, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakidaiwa kusafirisha kilo moja ya dawa za kulevya aina ya cocaine.
Washtakiwa hao ni Salum Kilindo (46), Salum Hassan (33) na Sofia Ngawaya (34).
Leo Ijumaa, Septemba 19, 2025, washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 22886 ya mwaka 2025, walisomewa shtaka lake na wakili wa Serikali, Michael Sindai, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Anna Magutu.
Kabla ya kusomewa shtaka hilo, hakimu Magutu alisema washtakiwa hawatakiwi kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi za uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali maalumu.
Pili, shtaka la kusafirisha cocaine zenye uzito huo halina dhamana kwa mujibu wa sheria, hivyo washtakiwa wataendelea kubaki rumande.
Akimsomea hati ya mashtaka, wakili Sindai alidai kuwa washtakiwa hao wanadaiwa kwa pamoja kutenda kosa hilo Agosti 11, 2025, eneo la Manzese. Siku hiyo ya tukio, wanadaiwa kusafirisha dawa za kulevya aina ya cocaine zenye uzito wa kilo 1.95 kinyume cha sheria.

Washtakiwa watatu wanaokabiliwa na shtaka la kusafirisha dawa za kulevya aina Cocaine, wakiwa chini ya ulinzi wa askari Polisi, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
Baada ya kusomewa shtaka lao, upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa. Hakimu Magutu ameahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 2, mwaka huu. Washtakiwa wamerudishwa rumande kwa sababu kesi inayowakabili haina dhamana kwa mujibu wa sheria.