Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imesema kuwa viongozi wa dini wana nafasi ya kipekee katika kuwaelimisha waumini kuhusu madhara ya rushwa, katika kipindi hiki kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025.
Taasisi hiyo imesema viongozi hao wana jukumu muhimu la kutokomeza rushwa kutokana na nafasi yao ya kuwaongoza wananchi wengi kupitia imani ya dini.
Kauli hiyo imetolewa leo Septemba 19, 2025 na Mkuu wa Takukuru Wilaya ya Ilala, Faustin Maijo, wakati wa semina maalumu kwa viongozi wa dini wa wilaya hiyo ikiwa ni juhudi za kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka huu.
Mafunzo hayo yanakuja wakati vyama vya siasa tayari vinaendelea kunadi sera kwa wananchi tangu Agosti 28, 2025 hadi Oktoba 28, 2025 kabla ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani.
“Kiongozi anayechaguliwa kwa kutumia rushwa si muadilifu, atakuwa na lengo la kurejesha fedha alizotumia badala ya kuhudumia wananchi kwa haki. Ndio maana tumewashirikisha viongozi wa dini ili kupitia wao, ujumbe huu uweze kuwafikia wananchi kwa wepesi zaidi,” amesema Maijo.
Ameongeza kuwa tayari kuna baadhi ya malalamiko kuhusu wagombea kukiuka kanuni, lakini mpaka sasa hakuna mgombea aliyebainika kujihusisha moja kwa moja na rushwa ya fedha.
Amewataka wagombea wote kuwa waangalifu na kuzingatia sheria, akisema yeyote atakayethibitika, hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.
Baada ya semina hiyo, Mchungaji Rukia Mwakenja kutoka Kanisa la Molovian, Ushirika wa Chanika amesema elimu waliyopewa na Takukuru ni muhimu kwao kama viongozi wa kiroho, kwani wanalo jukumu la kuelimisha kuhusu uovu wa rushwa.
“Rushwa ni adui wa haki. Hata maandiko ya kidini yanakataza rushwa. Tumejifunza mengi leo, na nitahakikisha nawasilisha ujumbe huu kwa waumini wangu ili wasishiriki wala kuunga mkono vitendo vya rushwa,” amesema Mchungaji Rukia.
Naye Said Hassani Mbwago, Mjumbe wa Baraza la Mashekhe Kata ya Pugu, amesema nafasi ya dini katika kupambana na rushwa ni kubwa, na kwamba mafundisho ya dini zote yanakataza vikali vitendo vya rushwa.
“Kila mwanasiasa ana dini, na dini zote zimekataza rushwa. Sasa tusikatae misingi ya dini zetu kwa ajili ya siasa. Ni jukumu letu kama viongozi wa dini kuwakumbusha waumini wetu kwamba kushiriki katika rushwa ni sawa na kujitafutia dhambi,” amesema Mbwago.
Amesema ataendelea kuwataka waumini wake kushikilia maadili na kukataa rushwa hasa katika kipindi hiki cha kampeni na uchaguzi.