BAADA ya dabi kumalizika na Simba kupoteza kwa mara ya sita mfululizo mbele ya Yanga, mjadala mkubwa kwa sasa ni kocha wa Wekundu wa Msimbazi, Fadlu Davids ikielezwa yupo mbioni kupigwa chini, lakini kumbe ukweli wa mambo wala sivyo ulivyo kama ilivyosambaa mtandaoni.
Tangu jana jioni kumekuwa na taarifa kwamba huenda Fadlu asirejee na kikosi hicho kutoka Botswana walikoenda kucheza na Gaborone United katika mechi ya Ligi ya Mabingwa kwa vile mabosi wamepoteza imani naye, lakini ukweli wa mambo umetua mezani kwa Mwanaspoti.
Inaelezwa ni kweli Fadlu anaweza kuondoka Msimbazi, lakini sio kwa kutimuliwa pengine kutokana na kupoteza mechi nne mfululizo mbele ya Yanga, ila ni kwa vile kuna ofa imeletwa mezani akitakiwa na klabu aliyowahi kuiona siku za nyuma kabla ya kuja Msimbazi.
Fadlu aliyeitumikia Simba tangu msimu uliopita akiweka rekodi ya kuifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ikipoteza mbele ya RS Berkane ya Morocco, inaielezwa aliongeza mkataba mpya wa mwaka mmoja na kutakiwa kubeba mataji yaliyokosekana Msimbazi kwa misimu minne iliyopita.
Kiwango ilichoonyesha Simba chini ya Fadlu imewafanya Raja Casablanca aliyokuwa akiinoa kama kocha msaidizi kabla ya kutua Simba, ijipange kumrudisha na tayari ofa hiyo ipo mezani na kwamba kocha huyo raia wa Afrika Kusini anasikiliziwa yeye kufanya uamuzi.
Taarifa za ndani zililiambia gazeti hili kuwa; “Fadlu sio kwamba anatakiwa kufukuzwa ila amepata ofa kubwa ya kutakiwa kurejea Morocco katika moja ya klabu kubwa. Licha ya ukubwa wa timu klabu hiyo imemuahidi kumlipa mshahara mara tatu ya ule alionao Simba, jambo ambalo limemuweka njia panda kocha huyo.”
Chanzo hicho kimeongeza kuwa, “Mabosi wa Simba walikuwa na mazungumzo naye ili abaki na sasa wanamsikilizia kwani aliwaambia bado hajafanya uamuzi wa mwisho na hajatoa jibu lolote hadi sasa kama atabaki au ataondoka Msimbazi.”
Mapema mwishoni mwa msimu kabla ya kupewa mkataba mpya, Mwanaspoti liliwahi kuandika kuwa, kocha huyo alipata ofa ya moja kati ya timu kutoka Sauzi na nyingine ya Afrika Kaskazini zikimhitaji ili kupata huduma yake msimu huu.
Hata hivyo, mabosi wa Simba kupitia bilionea wa klabu hiyo, Mohammed ‘MO’ Dewji walimalizana naye kwa kumpa mkataba mpya.
Kocha huyo amekuwa katika presha kubwa kutokana na kupoteza mechi ya Ngao ya Jamii ya pili mfululizo mbele ya Yanga kwa kulala 1-0, lakini hata katika Ligi Kuu msimu uliopita alipoteza mara mbili 1-0 na 2-0 na kuikosesha timu hiyo ubingwa wa Ligi na kutolewa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho ikifungwa na Singida BS iliyopoteza 2-0 mbele ya Yanga iliyotetea taji kwa mara ya nne.