OMO aahidi kuwashirikisha wananchi kuinua uchumi Zanzibar

Pemba. Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama cha ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman, maarufu OMO, amesema Serikali atakayoiunda itahakikisha kila mwananchi wa Pemba anashiriki katika shughuli za kiuchumi ili kukuza maendeleo ya kisiwa hicho.

Amesema wakazi wa Pemba hawatakiwi kufundishwa biashara, kwa sababu wana kipaji na uwezo, hivyo, Serikali ya ACT-Wazalendo itakayoundwa baada ya Oktoba 29, 2025 itawawezesha kushiriki katika uchumi.

“Tunataka wananchi wafaidike na uchumi wao, kama kuna jambo ambalo watu wanaweza kulifanya, basi walifanye. Kama hawawezi, tutawawezesha ili kuingia ubia na wengine watakaoweza, lakini lazima wananchi washiriki katika uchumi wa Taifa lao,” amesema Othman.

Othman ameeleza hayo leo Ijumaa, Septemba 19, 2025, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Jimbo la Ziwani, Pemba, katika mwendelezo wa kampeni za kusaka kura zitakazomhakikishia ushindi katika uchaguzi mkuu  utakaofanyika Oktoba 29.

Mgombea huyo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, amesema hoja ya wakazi wa Pemba kushiriki katika uchumi ipo katika mpango maalumu wa mambo 10 ya kuifungua Pemba kiuchumi na kimaendeleo.

“Mungu akijaalia, haya ndiyo yatakayoigeuza Pemba ili kuwa kisiwa cha neema sana. Ndugu, hakuna sababu ya kutokuwa ajira. Tutakwenda kupambana na, inshallah, Oktoba tutaifua Zanzibar na kuifungua Pemba,” amesema.

Awali, Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo (Zanzibar), Ismail Jussa, amedai kuanzia mwaka 2020 hadi sasa, wananchi wa Zanzibari wamekuwa wakilalamika kuhusu ongezeko la tozo na kodi katika maeneo mbalimbali.

“Hakuna aliyesalimika, kuanzia wakulima, wafugaji, wavuvi hadi wafanyakazi wa Serikali, hali ni mbaya. Tunayasema haya ni mjue kwamba fedha hizi zilipaswa ziwanufaishe maisha ya Wazanzibari.

“Serikali ya ACT-Wazalendo haiamini katika kuwakamua wananchi kwenye kodi. Leo wanajisifu kwa majengo, lakini mbona hali ni mbaya ebu angalieni huu umasikini. Hadi leo tunaishi kwenye nyumba za udongo, duniani makazi kama yamebakishwa kwenye makumbusho,” amesema Jussa.