Pemba. Mgombea wa urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wakulima (AAFP), Said Soud Said, amesema maono yake ni kuleta mabadiliko, iwapo wananchi wakimchagua atahakikisha anabadilisha maisha ya Wazanzibari, hususan wakulima wa karafuu.
Mgombea huyo ametoa kauli hiyo leo, Septemba 19, 2025, wakati akizungumza na viongozi, wananchi na wanachama wa chama hicho katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mchangamdogo, Kisiwani Pemba.
Amesema kwa sasa bei ya karafuu ni Sh15,000 kwa kilo ya gredi ya kwanza, lakini anataka kupandisha hadhi ya zao hilo.
Said amesema zao la karafuu limekuwa na bei kubwa duniani, hivyo, akipata ridhaa, ataliimarisha kwa kuongeza bei pamoja na kutoa vifaa na miche kwa wakulima.
Amesema ataanzisha vitalu vya miche ya mikarafuu katika maeneo tofauti na kuweka usimamizi mzuri ili kuona zao kuu la taifa linazalishwa kwa wingi na kuimarika.
“Mtakaponiichagua kuwa Rais wa Zanzibar, nitaimarisha kilimo cha karafuu kwa kuongeza bei kwa kilo hadi Sh50,000 kwa gredi ya kwanza na Sh40,000 kwa gredi ya pili. Pia nitaanzisha vitalu vya miche katika kila eneo, ili kila msimu wa mvua za masika unapofika, iweze kuoteshwa,” amesema Said Soud.
Makamu mwenyekiti wa chama hicho, Omar Juma Said, amewataka wananchi kutokubali kushawishiwa na wanasiasa kuvuruga amani iliyopo, kwani kunaweza kuhatarisha maisha yao.
Amesema vijana hawana budi kupuuza baadhi ya kauli zinazotolewa na wanasiasa zinazolenga kuhatarisha amani iliyopo nchini.
Naye mgombea mbunge wa Jimbo la Wawi, Khamis Haji Moh’d, akimnadi na kumuombea kura mgombea huyo wa urais, amewataka wananchi kuzingatia sera zao, kwani zimelenga kuboresha maisha ya wananchi wote.