Iringa. Kifo cha Frank Nyalusi, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa Jimbo la Iringa Mjini, kimeacha simanzi miongoni mwa wanachama wa chama hicho, viongozi wa kisiasa na wakazi wa Mkoa wa Iringa kwa ujumla.
Nyalusi amefariki dunia usiku wa kuamkia leo, Septemba 19, 2025, akiwa hospitalini kwenye chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu (ICU).
Akizungumza na Mwananchi leo, Septemba 19, 2025, katika Mtaa wa Mawelewele Bomba Mbili, Kata ya Mwangata, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, baba mdogo wa marehemu, Kassim Nyalusi, amesema familia imepata pigo kuondokewa na mpendwa wao.
“Marehemu ameacha mke mmoja na watoto wanne, wawili wakiwa wa kiume,” amesema Nyalusi.
Kifo hicho kimeongeza simanzi kwa kuwa Nyalusi amefariki dunia bila kufahamu kama mama yake mzazi, Pyela Mbata, naye alifariki dunia mapema mwezi huu, Septemba 3, 2025, baada ya kuugua kwa muda mfupi na kuzikwa katika makaburi ya Makanyagio, Kata ya Mkwawa, ambapo pembeni ya kaburi hilo ndipo atakapozikwa Nyalusi.
Viongozi, wanachama wa Chadema
Mwanachama mwandamizi wa Chadema, Patrick Sosopi, amesema amekosa maneno ya kuelezea msiba huo kutokana na ukubwa wa nafasi ambayo marehemu aliwahi kushika katika siasa na jamii.
Sosopi amesema chama hicho kilijitahidi kwa kila hali kupigania uhai wa Nyalusi, lakini jitihada hizo ziligonga mwamba kutokana na mapenzi ya Mungu.
“Tuliobaki tuna haki ya kupigania hali, uhuru na demokrasia ya chama chetu,” amesema Sosopi huku akihimiza kuendeleza mapambano ambayo marehemu alikuwa akiyaishi.
Akizungumza kuhusu marehemu, Sosopi amesema kila mmoja nchini ana jina lake la kumuita Nyalusi, jambo linaloashiria kuwa maisha yake yaligusa wananchi wengi.
“Lazima tukubali kwamba Nyalusi amefariki, ni miaka 15 tangu nimefahamiana naye nilipoanza siasa zangu mkoa huu wa Iringa,” amesema Sosopi.
Kwa upande wake, Katibu wa Chadema Kanda ya Serengeti, ambaye pia ni Mwenyekiti wa mazishi ya Nyalusi, Jackson Mnyawami, amesema msiba huo ni pigo kubwa kwa chama na taifa, kwani marehemu enzi za uhai wake alikuwa kiongozi shupavu na mwenye moyo wa kulinda haki za kila mmoja.
Mnyawami ameeleza kuwa kila mara chama kilipokumbana na changamoto, Nyalusi hakuwa nyuma, bali alijitokeza mstari wa mbele kuhakikisha chama kinabeba majukumu yake.
“Niwaombe wananchi wote tujitokeze kumzika na kumpumzisha ndugu yetu. Kiukweli nashindwa kusema mengi, kila mmoja nchini anamlilia Nyalusi kwa sababu ya utendaji wake ndani ya chama,” amesema Mnyawami.
Wakili wa marehemu, Emmanuel Chengula, amesema Nyalusi atakumbukwa zaidi kwa moyo wake wa kupigania wanyonge bila kuchoka na kwa uthubutu wa kulinda haki ya kila mmoja na Chadema.
“Marehemu alikuwa kiongozi wa kipekee, kwani alijitoa kwa moyo wote kwa watu wa kawaida. Aliwapigania bila kuchoka, na hakuwahi kuchagua upande wa kusimama katika suala la haki,” amesema Chengula.
Diwani wa Kata ya Mwangata
Diwani mstaafu na mgombea udiwani Kata ya Mwangata kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Gallus Lugenge, amesema msiba huo umemgusa kwa sababu aliwahi kushirikiana na Nyalusi katika harakati za kisiasa.
“Kipindi cha 2010 hadi 2015 tulishirikiana vizuri kwenye siasa, naweza kusema siasa hizo ndizo zinazohitajika kila wakati. Hata tukitofautiana kiitikadi, marehemu alikuwa mtu wa mshikamanano na mshauri mwema,” amesema Lugenge.
Maneno ya Lugenge yalionekana kugusa hisia za waliohudhuria msiba huo, kwani yalionesha kuwa hata nje ya vyama, Nyalusi aliheshimika kwa utu na ushirikiano wake.
Majirani wa marehemu walieleza kuwa Nyalusi alikuwa mtu mnyenyekevu, mwenye upendo na aliheshimu kila mtu katika jamii bila kubagua.
“Tulimfahamu Nyalusi kama jirani mwenye kujali, alishiriki nasi kwenye shida na furaha. Kwa kweli kifo chake kimetuacha na pengo kubwa,” amesema Happy Mgeni, jirani wa familia ya Nyalusi.
Baadhi ya wananchi wa Iringa walijitokeza msibani wakionesha mshikamano na familia, huku wengi wakikiri kuguswa na historia ya marehemu.
“Nyalusi alikuwa mwalimu wa jamii na hakika tulijifunza mengi kwake, hasa ujasiri na msimamo wa kupigania haki bila woga,” amesema Mussa Ally, mkazi wa Mkwawa.
Mmoja wa vijana wa Chadema, Daudi Mhagama, amesema marehemu alikuwa mfano wa kuigwa kwa viongozi vijana, kwa kuwa aliamini katika siasa safi na kuheshimu utu.
“Tulikuwa tunamchukulia kama mwalimu wetu na alitufundisha kuwa siasa si uhasama, bali ni chombo cha kuwatumikia wananchi,” amesema Mhagama.