WATUMISHI WIZARA YA NISHATI WAPATIWA ELIMU YA MATUMIZI SAHIHI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA.

………………..

📌 Ni baada ya Dkt.Biteko kuwakabidhi  majiko yanayotumia umeme kidogo (Induction Cookers).

📌 Yaelezwa kuwa majiko hayo yanatumia umeme kidogo kwa gharama ndogo

Watumishi wa Wizara ya Nishati leo wamepata  elimu ya matumizi bora na sahihi ya majiko yanayotumia umeme kidogo  ( Induction cookers) baada ya kukabidhiwa majiko hayo na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko hivi karibuni.

Dkt. Biteko aliwakabidhi majiko hayo Watumishi wa Wizara ya Nishati ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia na kwa kutambua kuwa Watumishi hao ni mabalozi katika utoaji wa elimu ya Nishati Safi ya Kupikia kwa wananchi.

Mafunzo hayo ambayo yamefanyika katika Ofisi za Wizara ya Nishati- Mtumba,  Dodoma yameandaliwa na Kitengo cha Nishati safi ya kupikia kwa kushirikiana na wataalam kutoka Kampuni ya Positive Cooker.

Akitoa elimu ya matumizi bora na sahihi ya majiko hayo,  Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni  ya Positive Cooker, Ndg. Atukuzwe Willson ameeleza kuwa lengo la utoaji wa mafunzo hayo ni sehemu ya uhamasishaji  wananchi kutumia umeme kwa matumizi ya kupikia  kupitia majiko janja yanayotumia umeme kidogo.

“Lengo la kutoa elimu hii ni kuhakikisha  kila Mtanzania anaachana na matumizi ya nishati isiyosafi ili kulinda mazingira pamoja na   afya zetu lakini pia ni  sehemu ya jitihada za kuunga mkono kampeni ya nishati safi ya kupikia ambapo hadi kufikia mwaka 2034 asilimia 80 ya  watanzania wanapaswa kutumia nishati safi ya kupikia.” Amesema Willson

Akizungumza kuhusu  majiko hayo janja ya umeme amesema  yanatumia wastani  wa nusu uniti hadi uniti moja na nusu kwa wastani wa dakika 15 mpaka dakika 90 sawa na shilingi 65 mpaka shilingi 534 tu hali inayothibitisha ufanisi wa majiko hayo kuwa na  gharama nafuu, kuokoa muda, kulinda afya pamoja na mazingira.