Mkutano wa NCCR-Mageuzi Sumbawanga wakwama, sababu yarajwa

Rukwa. “Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia NCCR-Mageuzi, Ambari Haji Hamisi, ameshindwa kuhutubia mkutano wa kampeni katika viwanja vya Sabato Jangwani, Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa, baada ya kujitokeza wananchi wachache.

Tukio hilo limetokea baada ya wananchi kutojitokeza kwa wingi kama ilivyotarajiwa. Hata hivyo, mkutano uliendelea kwa kuhutubiwa na wagombea wawili wa udiwani wa kata za Momoka na Msua.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa viongozi wa chama hicho mkoani humo, pamoja na kuwepo kwa maandalizi ya kutosha katika eneo la tukio, idadi ndogo ya watu waliojitokeza ilisababisha uamuzi wa kuahirisha kampeni hiyo.

Akizungumza na Mwananchi leo, Septemba 19, 2025, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Mkoa wa Rukwa, Patrick Mbalamwezi, amethibitisha kutofanyika kwa mkutano huo wa kampeni, akieleza kuwa uamuzi huo ulifikiwa kutokana na kutokuwepo kwa mahudhurio ya kutosha kutoka kwa wananchi.

“Ni kweli mgombea wetu alikuwepo kwa ajili ya kuhutubia mkutano wa kampeni, lakini kwa bahati mbaya wananchi hawakujitokeza kwa idadi iliyotarajiwa.

“Tutajipanga wakati mwingine ili kuhakikisha tunawahamasisha wananchi wajitokeze kusikiliza sera na kunadi wagombea udiwani kupitia chama chao,” amesema Mbalamwezi.

Kwa upande wake, mgombea udiwani Kata ya Momoka, Paulo John Kusaya, amewaomba wananchi waliokuwepo wajitokeze kumpigia kura na kwamba akishinda atawajengea zahanati katika kata hiyo na kuhakikisha wanapata huduma bora za afya.

“Nikipata ridhaa ya kuchaguliwa nitahakikisha soko la mazao linajengwa na pia tunatengeneza miundombinu ya barabara katika kata yetu,” amesema Kusaya.

Naye mgombea udiwani kutoka Kata ya Msua, Julius Lazaro Mwandele, amewataka wananchi na wanachama kutofanya makosa ifikapo Oktoba 29, 2025, kuhakikisha wanampigia kura pamoja na mgombea urais kupitia tiketi chama hicho.

Baadhi ya wananchi waliojitokeza katika mkutano huo wa kampeni, akiwemo Maufi Maufi, wamemwomba mgombea huyo pindi atakapopata ridhaa ahakikishe anawajengea zahanati katika kata hiyo.

“Nikuombe mgombea, ukipata nafasi hapo Oktoba, usimamie ujenzi wa zahanati pamoja na miundombinu ya barabara ni mibovu, wewe mwenyewe umeiona na umepita. Tusaidie tupate barabara nzuri,” amesema.