::::::::
Mjumbe Maalum wa Umoja Wa Afrika wa Masuala ya
Wanawake, Amani na Usalama, Balozi Liberata Mulamula amesisitiza umuhimu wa amani nchini hususan kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29.
Balozi Mulamula ametoa rai hiyo jijini Dodoma leo, alipoungana na jamii ya kimataifa kuadhimisha Siku ya Amani Duniani ikiwa ni fursa ya kutafakari umuhimu wa amani kwani ndiyo msingi wa maendeleo na mafanikio kama ulivyo msisitizo wa Mhe. Rais Dk.Samia Suluhu Hassan.
“Tunapoungana na jamii ya kimataifa ya kuadhimisha Siku ya Amani Duniani ni fursa ya kutafakari umuhimu wa amani tunapoelekea Uchaguzi Mkuu. Tuthibitishe dhamira yetu ya pamoja ya kujenga, kuilea na kudumisha amani yetu kama alivyosisitiza Mhe. Rais Dkt. Samia katika hotuba yake wakati wa kuzindua Kampeni yake ya Uchaguzi huko Zanzibar,'”alieleza.
“Kwetu sisi hapa Tanzania hii ni fursa ya kuimarisha mfumo wetu wa kitaifa wa amani kuhakikisha kuwa mitazamo, vipaumbele, na uongozi wa wanawake vinajumuishwa katika ngazi ya jamii. Na kwamba Tanzania imeendelea kuwa mfano wa amani na utulivu katika Bara la Afrika,” amesisitiza.
Alisema dhamira ya Umoja wa Afrika ni kushirikisha Wanawawake na Vijana katika kuleta amani endelevu na kudumisha umoja wa Bara la Afrika.