SIMBA imetabiriwa inaweza kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, lakini iwapo tu, wachezaji wa timu hiyo watakuwa tayari kupambana kwa jasho na damu wakijengwa na utulivu utayari, uzalendo na kulinda viwango vyao kwa kuzingatia vitu vya msingi.
Ujanja huo umetolewa na nyota wa zamani wa kikosi hicho, Mzambia Moses Phiri alipozungumza na Mwanaspoti na kusema amekuwa akikifuatilia kikosi cha Simba na kubaini kuna wakali kibao wanaoweza kuibeba zaidi ya msimu uliopita.
Nyota huyo anayekipiga kwa sasa Green Eagles ya Zambia, alisema mastaa wa Simba wanapaswa kujua jukumu walilonalo ni kutengeneza furaha ya mashabiki wa klabu hiyo maarufu Afrika.
Phiri alisema uzoefu ilionayo Simba katika michuano ya CAF, anaiamini ina nafasi ya kufika mbali kuliko fainali ya Kombe la Shirikisho iliyocheza msimu uliopita na kupoteza kwa RS Berkane ya Morocco kwa mabaa 3-1.
Alisema aliiona Simba ikicheza dhidi ya Yanga katika mechi ya Ngao ya Jamii kupitia mitandao ya kijamii, wachezaji walionyesha kiwango kizuri, hivyo inaweza ikafikia hatua kama msimu uliopita ilipocheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
“Kufungwa bao 1-0 dhidi ya Yanga hakuondoi ubora wa kikosi hicho, niliona msimu uliopita ilipoteza mechi zote za dabi lakini ikawa na mafanikio makubwa CAF,” alisema Phiri aliyefunga mabao 10 msimu wake wa kwanza (2022/23) na mabao matatu kabla hajaondoka Januari 2024 kwenda kujiunga na Power Dynamos.
Staa mwingine wa zamani wa timu hiyo, Meddie Kagere alisema Simba ina uzoefu mkubwa wa kucheza michuano ya CAF, hivyo anaamini itafanya vizuri kwa mwaka huu.
“Viongozi wasajili wachezaji wenye viwango vya juu, kama ilivyokuwa kipindi chetu kila nafasi ilikuwa na ushindani mkali, mfano ya ushambuliaji nilikuwapo mimi, Chris Mugalu, John Bocco, Luis Miquissone na Emmanuel Okwi ambaye sikucheza naye kwa muda mrefu akaondoka, makocha walikuwa wana uhakika wa kupata mabao muda wowote,” alisema.
Kagere alisema timu hiyo inahitaji utulivu na kuwapa wachezaji muda wa kuzoeana.
“Utayari wa mchezaji ni kuweka akili yake na nguvu katika kazi, mfano nilipokuwa nina majukumu ya mechi mbele yangu, basi nilikuwa napumzika mapema kuupa mwili nguvu, mambo ya mitandao kulala usiku wa manane haikuwa sehemu ya maisha yangu pia kuwa wazalendo kwa timu ni kujitolea kwa namna yoyote ile ili kupata ushindi,” alisema.
Kwa upande wa aliyekuwa kiraka wa timu hiyo, Erasto Nyoni alisema: “Simba ina nafasi ya kufanya makubwa katika michuano ya CAF, jambo la msingi ni utulivu, utayari na kujitoa kwa wachezaji hapo kila kitu kitakwenda vizuri.”
Ligi Kuu Kagere aliifungia Simba (2018-2019)-Mabao (23), (2019-2020)-Mabao (22), (2020-2021)-Mabao (13) na (2021-2022)-Mabao (7)