JKT Tanzania yaipigia hesabu Coastal Union

BAADA ya kuanza msimu mpya wa Ligi Kuu kwa kupata sare ya 1-1 ugenini dhidi ya Mashujaa, maafande wa JKT Tanzania wameanza hesabu mpya za kubeba alama kutoka kwa Wagosi wa Kaya watakaokutana nao keshokutwa Jumatatu jijini Tanga.

Kocha wa maafande hao, Ahmad Ally alisema katika soka kuna nyakati za kiuchezaji kulingana na mechi husika wanazozitumia  kuhakikisha timu inapata matokeo ya ushindi na hili ndilo lililotokea kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, mjini Kigoma dhidi ya Mashujaa.

Ally aliliambia Mwanaspoti, mechi dhidi ya Mashujaa ilikuwa ngumu na yenye ushindani, hivyo ilihitaji kutumia mbinu na ufundi vilivyowafanikisha kuwapa pointi moja na sasa wanajipanga kwa mechi ya Coastal Union itakayopigwa Jumatatu.

“Mashujaa ina wachezaji wenye uwezo mkubwa, benchi la ufundi imara na viongozi wanaoisapoti timu, ndivyo ilivyo kwa JKT Tz, hilo lilichangia mechi kuwa ngumu na yenye ushindani kwa wachezaji,” alisema kocha Ally na kuongeza;

“Kilichoamua timu zigawane pointi moja moja ni mbinu tulizotumia makocha, hilo linaonyesha namna ambavyo msimu huu utakuwa mgumu, timu zimejisajili na zimefanya maandalizi ya kutosha.”

Kocha huyo alisema kwa sasa wanajiandaa dhidi ya Coastal mechi itakayopigwa Septemba 22, kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga na kikubwa anachokifanya ni kuzijenga akili za wachezaji ziwe na utayari wa kupambania pointi tatu.

Kwa upande wa kocha wa Mashujaa, Salum Mayanga alisema: “Kwa sasa tunajiandaa na mechi dhidi ya Mtibwa Sugar itakayochezwa Septemba 21, malengo yetu ni kuzipambania pointi tatu.”