Binti wa Rais Paul Biya Amuomba Umma Wasimpigie Kura Baba Yake – Global Publishers



Yaoundé – Dunia imetaharuki baada ya Brenda Biya, binti wa Rais wa Cameroon Paul Biya, kuwataka wananchi wa nchi hiyo wasimpigie kura baba yake katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.

Kupitia video aliyoipakia kwenye TikTok, Brenda anayejulikana mtandaoni kama “King Nasty”, alimlaumu baba yake kwa kusababisha umasikini wa wananchi, ukosefu wa ajira na kudorora kwa maendeleo nchini humo.

Tukio hili limeelezwa kuwa la kwanza barani Afrika ambapo mtoto wa rais aliye madarakani anampinga waziwazi mzazi wake kisiasa.

Rais Paul Biya, mwenye umri wa miaka 92, amekuwa madarakani tangu mwaka 1982, akitazamwa na wengi kama mmoja wa viongozi waliodumu madarakani kwa muda mrefu zaidi duniani.

Hata hivyo, wakosoaji wamesema kuwa Brenda, ambaye anaishi ughaibuni kwa maisha ya kifahari, hana uhusiano wa karibu na familia yake na huenda kauli yake isiakisi kwa usahihi hali halisi ya wananchi wa Cameroon.

Kwa sasa kauli hiyo imeibua mjadala mpana ndani na nje ya Cameroon, ikitazamwa kama changamoto ya kipekee kwa urithi wa kisiasa wa Rais Biya.