Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi, jana amezindua rasmi mbio za magari za Mkwawa Rally of Tanzania 2025 zinazofanyika mkoani Morogoro, ambapo madereva kutoka nchi mbalimbali wanachuana kusaka ubingwa wa African Rally Championship (ARC).
Uzinduzi huo ulifanyika kwenye viwanja vya mashamba ya mkonge Tungi, Morogoro, ambapo Profesa Kabudi amesema mashindano hayo yataamua dereva atakayekuwa kinara wa Afrika mwaka huu.
“Serikali inapongeza Mkurugenzi wa Mkwawa Group of Companies, Ahmed Huwel, kwa kudhamini mashindano haya kwa moyo wa kizalendo. Kupitia michuano hii, fursa nyingi za ajira zimefunguliwa kwa vijana, wanawake na wajasiriamali mbalimbali, huku pia uchumi wa eneo letu ukikua,” amesema Profesa Kabudi.
Waziri huyo ameongeza, mashindano hayo ni sehemu ya kutangaza vivutio vya ndani na kuimarisha michezo nchini. Alikiri kutamani kujaribu kupanda gari la mashindano, lakini akasema alichelea dhahama kutokana na kasi yake.
Kwa upande wa Rais wa Shirikisho la Mbio za Magari Tanzania (AAT), Nizar Jivan, amesema wanaendelea kushirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Baraza la Michezo Tanzania (BMT) ili kuendeleza mchezo huo.
“Mchezo huu una mashabiki wengi, hivyo tunaomba serikali kuendelea kusaidia kukuza mchezo huu. Ahmed Huwel ameonyesha mfano bora kwa kudhamini mbio hizi,” amesema Jivan.
Zaidi ya madereva 20 wanashiriki mbio hizo wakisaka taji la ubingwa wa Afrika, huku Tanzania ikiwa na madereva chipukizi wanaowania pia nafasi ya ubingwa wa taifa kupitia National Rally Championship.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Mbio za Magari Tanzania, Michael Maluwe, amesema mpambano mkali unatarajiwa kati ya Yassine Nasser na Samman Vohra, ambao wanaongoza msimu huu wa ARC. Kwa upande wa Tanzania, mashindano haya ni mzunguko wa nne ya kumpata bingwa wa taifa.
Kivutio kikubwa ni bingwa mtetezi, Manveer Birdi, anayekabiliwa na changamoto kutoka kwa kaka yake, Randeep Singh, wote wakiwa na magari ya Mitsubishi Evo 09. Washiriki wengine wanaotarajiwa kutoa ushindani ni Gurpal Sandhu (Mitsubishi Evo 10) na Ahmed Huwel (Toyota Yaris R5).
Mashindano haya yameibua msisimko mkubwa kwa wakazi wa Morogoro na mashabiki kutoka sehemu mbalimbali waliomiminika kushuhudia mbio hizo za kasi na ujanja wa madereva.