Askofu mstaafu Munga wa KKKT afariki dunia

Tanga. Askofu mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dk Stephen Munga amefariki dunia.

Akizungumza na Mwananchi, mke wa marehemu, Mchungaji Dk Anneth Munga, amesema kuwa Askofu Munga amefariki dunia leo Jumamosi, Septemba 20, 2025, majira ya saa 9:30 alfajiri akiwa katika Hospitali ya Rabinisia, jijini Dar es Salaam, ambako alikuwa anaendelea na matibabu.

“Baba Askofu ameaga dunia saa 9:30 alfajiri ya leo katika hospitali ya Rabininsia iliyopo hapa jijini Dar es Salaam, taarifa za mipango ya mazishi zitatolewa baadaye,” amesema Mchungaji Anneth Munga.

Msaidizi wa Askofu huyo, Mchungaji James Mwinuka amesema taarifa ya wapi atazikwa zitatolewa baada ya vikao, pale ndugu na jamaa zake watakapokutana kujadili ni wapi wataamua mazishi yakafanyike.

“Tutawaeleza kama atazikwa nyumbani kwake Kijiji cha Maramba Wilaya ya Mkinga, Tanga au kwingineko hii ni baada ya vikao baada ya familia kukutana na kujadili,” amesema Mchungaji Mwinuka.

Askofu Munga alihudumu nafasi ya askofu katika Dayosisi hiyo kuanzia mwaka 2001 hadi mwaka 2020.

Endelea kufuatilia Mwananchi