:::::::::
ALIYEWAHI kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii Lazaro Nyalandu ni kama vile ‘amewasha moto’ katika kumnadi na kumtafutia kura Mgombea wa Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na mgombea mwenza Dkt Emmanuel Nchimbi.
Hatua hiyo inatokana na ziara yake akiwa na baadhi ya vijana wake kuzunguka na kufanya kampeni mikoa mbalimbali ambayo wagombea hao wanapita kuomba kura, jambo ambalo wanachama wengi wamesema kuwa linapaswa kuigwa na wanachama wengine wakiwemo waliowahi kugombea nafasi za Ubunge hata Udiwani.
Huku akitumia basi maaalumu likinakshiwa rangi ya Chama hicho pamoja na Picha kubwa ya Dkt Samia, Timu hiyo ya Nyalandu imekuwa ikipita Wilaya kwa Wilaya na kukutana na viongozi na wanachama pamoja na wananchi mbalimbali na kuwaelezwa umuhimu wa kumpigia kura Dkt Samia siku ya uchaguzi Oktoba 29.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wanachama wa hicho mbali na kumpongeza wamesema hatua yake hiyo inatokana na mapenzi aliyonayo kwa Dkt Samia, CCM na Tanzania kwa ujumla kwani kabla ya hapo alikuwa akipita maeneo mbalimbali na kutangaza uzalendo.
” Huyu ni Kiongozi wa kuigwa, ukweli anaonesha mapenzi ya kweli kwa Rais, wapo baadhi baada ya kumalizika kwa mchakato wa kuwapata wagombea wamepotea kabisa hata hawaonekani majukwaani kuwaunga mkono wenzao, Nyalandu katoka huko na anaonekana kuwa ni mwanasiasa aliyeiva” amesema mmoja wa wanachama