Mwanza. Idadi ya ripoti za maudhi na madhara yatokanayo na matumizi ya dawa, chanjo, vifaa tiba na vitendanishi nchini imeongezeka kwa kasi, kutoka ripoti 200 mwaka 2020 hadi zaidi ya 10,000 kwa mwaka, kwa mujibu wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA).
Kwa mujibu wa TMDA, ongezeko hilo linatokana na uhamasishaji uliofanyika kwa watumiaji na watoa huduma za afya kuhusu umuhimu wa kuripoti madhara yanayotokana na bidhaa za afya, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kudhibiti usalama na ubora wa dawa na vifaa tiba nchini.
Imeelezwa madhara yanayotokana na dawa, chanjo, vifaa tiba na vitendanishi vinavyosambazwa sokoni na kutolewa katika vituo vya kutolea huduma nchini ni pamoja na mzio, maumivu ya kifua, ulemavu wa muda au wa kudumu na katika baadhi ya matukio, husababisha vifo.
Takwimu hizo zimetolewa Septemba 19, 2025, jijini Mwanza na Mkurugenzi wa mafunzo ya muda mfupi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), Dk Betty Maganda wakati wa mafunzo maalumu ya kuwajengea uwezo wataalamu wa afya, wakiwemo madaktari, wafamasia, wauguzi na watafiti, ili waweze kuripoti kwa usahihi maudhi na madhara yanayotokana na bidhaa za afya.

Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba (TMDA), Venance Burushi (wa pili kushoto) akimpongeza mshiriki bora wa mafunzo ya ufuatiliaji maudhi ya dawa, Nyegoro Magoti (kulia), jana jijini Mwanza. Picha na Damian Masyenene
Dk Betty amesema ongezeko kubwa la ripoti za maudhi na madhara kutoka ripoti 200 mwaka 2020 hadi zaidi ya 10,000 kwa mwaka, linatokana na juhudi za pamoja kati ya Muhas na TMDA, ambazo zimehusisha utoaji wa mafunzo kwa watumishi wa afya, waagizaji wa dawa, wazalishaji, pamoja na taasisi za utafiti nchini.
“Baada ya kufanya utafiti, tuligundua kuwa tatizo kubwa lilikuwa ni ukosefu wa uelewa kuhusu namna ya kujaza taarifa za maudhi na kuzifikisha TMDA. Tangu mwaka 2020, tulianzisha mafunzo haya na hadi sasa zaidi ya wakufunzi 400 nchini wameshapatiwa mafunzo haya maalumu,” amesema Dk Betty.
Ameongeza kuwa kupitia mafunzo hayo, wataalamu wapatao 45 waliopo katika eneo hilo wataweza kujaza kwa usahihi taarifa za maudhi na madhara ya dawa zinazotolewa katika vituo vya kutolea huduma, taarifa ambazo zitafikishwa TMDA na pia kuwasilishwa kwa Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa uchambuzi na hatua zaidi.
”Tunaamini baada ya kutoka hapa watakuwa mabalozi wazuri wa kujaza fomu za maudhi mbalimbali ya dawa, chanjo, vifaa tiba na vitendanishi ili kuhakikisha taarifa hizo zinafika TMDA na WHO ili kama kuna shida yoyote katika dawa zetu wachukue hatua stahiki,” amesema Dk Betty.

Mkurugenzi wa mafunzo mafupi ya Pharmacovigilance kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), Dk Betty Maganda akizungumza na watumishi wa afya waliohudhuria mafunzo hayo (hawapo pichani) jana jijini Mwanza. Picha na Damian Masyenene
Naye, Kaimu Meneja wa TMDA Kanda ya Ziwa Mashariki, Venance Burushi amesema elimu hiyo ni eneo muhimu katika kufuatilia na kuratibu usalama wa watumiaji wa bidhaa za dawa, chanjo, vifaa tiba na vitendanishi katika soko baada ya kusajiliwa na kuidhinishwa kwa matumizi.
Burushi amesema licha ya dawa kufanyiwa majaribio, zinapoingia sokoni matokeo ya matumizi yake yanaweza kutofautiana na ya kwenye majaribio na kuleta maudhi mbalimbali kwa watumiaji ikiwemo maumivu, kusabaisha vifo na ulemavu.
“Baada ya dawa kudhibitishwa inabidi iendelee kufanyiwa ufuatiliaji katika soko, na watu walio msitari wa mbele ni pamoja na tuliowapa mafunzo leo, ambao watafuatilia huo ubora, usalama na ufanisi katika soko baada ya kuanza kutumika katika vituo vya kutolea huduma,” amesema Burushi.
Amesema kama wataalamu hao wa afya watatimiza wajibu wao baada ya kupata elimu hiyo itakuwa rahisi kupata taarifa za bidhaa zinazoleta changamot katika soko ili zifanyiwe tathmini na kuchukua hatua stahiki.
”Matarajio yetu ni kwamba hawa washiriki wataenda kuongeza tija katika kukusanya taarifa za matukio yanayotokana na matumizi ya hizo bidhaa na kuziwasilisha TMDA kwa wakati, ili kuchukua hatua mapema na kunusuru watu wengi,” amesema Burushi.
Nyegoro Magoti, mfamasia wa Hospitali ya Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, amesema mafunzo hayo yamewapa mbinu mpya za kufuatilia ubora wa dawa na chanjo.
“Tulikuwa haturipoti sana madhara ya dawa, lakini sasa nitawaelimisha wenzangu ili tuweze kutuma taarifa kwa wakati na kusaidia kuondoa dawa hatarishi sokoni,” amesema Nyegoro.
Naye, Noel Chacha, mfamasia kutoka Hospitali ya Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), amesema elimu hiyo inapaswa kuingizwa kwenye mitalaa ya vyuo vya afya.
“Ni maarifa muhimu sana kwa wanafunzi wa udaktari na famasia, nashauri elimu hii iingizwe kwenye mitalaa kila mhitimu atakuwa anajua wajibu wake mapema,” amesema.