Moshi. Mabalozi 12 kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya (EU) wametembelea Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro (Kinapa) na kueleza kuwa zinahitajika jitihada za makusudi kunusuru barafu ya Mlima Kilimanjaro, ambayo imeendelea kupungua kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza katika lango la Marangu, jana Septemba 19, 2025 wakati wa kuhitimisha ziara ya siku tatu mkoani Kilimanjaro, Balozi wa Finland nchini Tanzania, Theresa Zitting amesema kupungua kwa barafu kunaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa mazingira, utalii na maisha ya jamii zinazotegemea rasilimali za mlima huo.
Amesema kupungua kwa barafu ni ishara ya wazi ya mabadiliko ya tabianchi yanayoikumba dunia, hivyo zinahitajika jitihada za pamoja kunusuru hali hiyo.
Balozi huyo amesema ni jambo la kusikitisha kushuhudia jinsi barafu inavyopungua na namna hali hiyo inavyotarajiwa kuathiri mtiririko wa maji na mfumo wa ikolojia katika maeneo ya chini ya mlima.
“Tatizo hili si la Tanzania pekee, hata Finland tunashuhudia mabadiliko ya joto,” amesema.
Balozi Zitting amesema watalii 60,000 hutembelea Hifadhi ya Kilimanjaro kila mwaka, wengi wao kutoka nchi wanachama wa EU.

Balozi wa Finland nchini Tanzania, Theresa Zitting akizungumza wakati walipotembelea hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro.
Balozi wa EU nchini, Christine Grau, amesema umoja huo umejipanga kuendeleza ushirikiano na Tanzania kupitia sera za Green Deal zinazolenga kufikia sifuri ya hewa ya ukaa na kutimiza malengo ya Mkataba wa Paris.
Ofisa Uhifadhi Mwandamizi na Mkuu wa Kitengo cha Utalii Kinapa, Stephen Moshy amesema ujio wa mabalozi hao umewapa nafasi ya kueleza vivutio vilivyomo katika hifadhi, shughuli za utalii zinazofanyika na mchango wa hifadhi hiyo kwa jamii zinazozunguka mlima.
Amesema ziara hiyo ina umuhimu mkubwa katika kuhamasisha utalii na kuongeza uelewa wa kimataifa kuhusu hifadhi hiyo.
“Tumeweza kuzungumza nao kuhusu changamoto tunazopitia, ikiwamo suala la teknolojia ya vyoo mlimani kwani vilivyopo haviendani na mahitaji ya sasa. Wameonyesha nia ya kushirikiana nasi ili kuboresha miundombinu hiyo. Lakini zaidi, ujio wao una taswira kubwa kwa sababu wanawakilisha nchi zao 12, hivyo wakirudi wakitoa taarifa kwa wananchi wao tunaamini utaleta hamasa na ongezeko kubwa la watalii,” amesema Moshy.
Kwa upande wake, Ofisa Uhifadhi Mkuu ambaye ni Kaimu Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro, Amri Mtekanga, amesema wageni hao wamejifunza kuhusu shughuli za utalii, ikolojia na usimamizi wa mazingira, huku akisisitiza umuhimu wa kuimarisha jitihada za pamoja katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
“Mlima Kilimanjaro ni chanzo kikuu cha maji yanayotumika katika mikoa ya Kilimanjaro na Tanga. Tukifanikiwa kuendelea kulinda barafu ya kilele cha mlima huu, tutaendelea pia kuhakikisha upatikanaji wa maji kwa vizazi vya sasa na vijavyo,” amesema.
Hali ya asili katika Mlima Kilimanjaro inatajwa kubadilika kadri miaka inavyosonga, sababu kubwa ikitajwa ni mabadiliko ya tabianchi.
Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro ina eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 1,688 ambalo ndani yake lina uoto na wanyama ambao ni kivutio cha utalii.
Kwa mujibu wa jarida la Ujirani Mwema la Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) la Januari hadi Machi, 2023 tafiti zinaonyesha kutoweka kwa barafu iliyo katika kilele cha Mlima Kilimanjaro iwapo hatua madhubuti za kudhibiti mabadiliko ya tabianchi hazitachukuliwa.
Kwa mujibu wa tafiti hizo, jarida hilo linaeleza tangu mwaka 1912 kumbukumbu za mlima huo zilipoanza kuhifadhiwa, barafu imekuwa ikipungua kwa wastani wa nusu mita kila mwaka na kubashiri kuwa huenda ikaisha kabisa ifikapo mwaka 2050.
Miongoni mwa sababu zinazotajwa kusababisha hali hiyo ni kuongezeka joto duniani kunakotokana na shughuli za kibinadamu na uchomaji moto katika Mlima Kilimanjaro.