Mbeya. Sekondari ya Wasichana Joy ni taasisi binafsi changa yenye dira kubwa katika sekta ya elimu nchini Tanzania. Inamilikiwa na Titho Tweve, ambaye pia ndiye Mkurugenzi Mkuu.
Shule hii imejipambanua kuwa nguzo ya elimu bora sambamba na malezi ya kiroho kwa watoto wa kike.
Akizungumza na Mwananchi, Meneja wa shule, Augustino Daudi, anasema taasisi hii ni ya bweni pekee na imesajiliwa na Wizara ya Elimu kwa namba S.5612.
Ilianzishwa mwaka 2022 na licha ya uchanga wake, tayari imeonesha mafanikio makubwa na kujipatia heshima ndani ya jamii.

Awali, lengo lilikuwa kudahili wanafunzi 90 katika mikondo miwili ya wanafunzi 45 kila mmoja, lakini shule ilianza na wanafunzi 44 pekee. Baada ya muda mfupi, idadi ikaongezeka kufikia 50, ambao ndio wa kwanza kuhitimu mwaka huu.
Meneja huyo anasema hatua hiyo ni ushuhuda wa imani kubwa ya wazazi, walezi na wadau waliowaamini.
“Mungu awabariki sana kwa kutuweka katika nafasi hii,” anasema Daudi kwa unyenyekevu.
Kwa sasa, shule ina jumla ya wanafunzi 299, kati yao 50 wako kidato cha nne, 77 kidato cha tatu, 79 kidato cha pili na 93 kidato cha kwanza. Takwimu hizi zinaonesha kasi kubwa ya ukuaji wa taasisi hiyo.
Kwa upande wa rasilimali watu, shule ina wafanyakazi 35, wakiwamo walimu 17 waliobobea katika taaluma zao na wafanyakazi wasio walimu 18 wanaosaidia shughuli mbalimbali za kila siku.
Meneja Daudi anasisitiza kuwa walimu hao wana uzoefu mkubwa na moyo wa kujitolea kuhakikisha kila mwanafunzi anapata elimu bora.
“Tunawashukuru walimu wetu kwa moyo wa kujitolea, hakika ni nguzo kubwa ya mafanikio,” anasema.
Sekondari ya Joy inawakaribisha wanafunzi kutoka ndani na nje ya Tanzania, jambo linaloonesha kuwa taasisi hii ina mtazamo wa kimataifa na inalenga kufanikisha ndoto za watoto wa kike bila mipaka ya kijiografia.
Shule haina ubaguzi wa dini wala imani. Wanafunzi kutoka madhehebu yote wanapokewa na kulelewa kwa misingi ya kiroho kupitia kanuni za Kanisa la Waadventista Wasabato.

Kwa kufanya hivyo, shule inalenga kuandaa viongozi wenye maadili, hekima na maarifa watakaosaidia jamii ndani na nje ya nchi.
Pia, shule imeweka mkakati wa kuhakikisha kuwa mwanafunzi akianza masomo anamaliza, bila kujali changamoto zinazoweza kumpata.
Hata ikitokea msiba wa mzazi au ugumu wa ada, uongozi huingilia kati kuhakikisha elimu haikatishwi.
Kwa familia zinazokaa karibu na shule, ada imepunguzwa kwa asilimia 30 ili kupunguza gharama na kuwapa watoto nafasi ya kupata elimu bora.
Meneja Augustino anaeleza kuwa miundombinu ya shule ni ya kisasa na rafiki kwa mtoto wa kike, yakiwamo madarasa ya kutosha na mabweni yenye uwezo wa kuhifadhi zaidi ya wanafunzi 450.

Meneja wa shule ya Sekondari ya Wasichana Joy, Augustino Daudi.
Usalama pia umeimarishwa kwa ukuta imara na kamera za CCTV zilizowekwa maeneo yote muhimu, hatua inayowawezesha wanafunzi kujikita zaidi katika masomo bila hofu ya changamoto za nje.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Titho Tweve anasema shule imejiwekea malengo makuu matatu:
Kwanza, kuletea ukombozi wa fikra mtoto wa kike.
Pili, kutoa elimu bora itakayowawezesha wanafunzi kufaulu kwa kiwango cha juu kwenye mitihani ya kitaifa.
Tatu, kukuza vipaji na maadili ya wanafunzi kupitia mashindano na shughuli mbalimbali za kiimani.
Mwalimu wa Taaluma, Michael Irody, anabainisha kuwa kaulimbiu ya shule ni “Elimu bora kwa Utukufu wa Mungu” ambayo imekuwa dira ya kila jitihada za walimu na wanafunzi.

Kuhusu ufaulu, anasema katika mtihani wa kidato cha pili mwaka 2023, wanafunzi 44 walipata daraja la kwanza na mmoja tu alipata daraja la pili.
Mwaka 2025, wanafunzi wa kidato cha nne walifanya mtihani wa utimilifu wa kanda na wote walipata daraja la kwanza.
Matokeo hayo yalihusisha shule kutoka mikoa ya Mbeya, Songwe, Ruvuma, Katavi na Njombe, ambapo Joy ilishika nafasi ya kwanza kiwilaya kati ya shule 34, nafasi ya pili kimkoa kati ya shule 205 na nafasi ya saba kikanda kati ya shule 581.
Mafanikio hayo yamewajengea ujasiri kwamba, katika mtihani wa Taifa wa mwaka 2025, wanafunzi wote watafaulu kwa daraja la kwanza.
Mbali na masuala ya kitaaluma, shule inashiriki mashindano ya mdahalo na hotuba ndani na nje ya Tanzania. Mwaka huu, wanafunzi wanatarajiwa kushiriki mashindano ya Afrika yatakayofanyika Botswana, Desemba 2025.
Pia hufanya ziara za kitaaluma ndani na nje ya nchi, hatua inayopanua upeo wa maarifa kwa wanafunzi.
Katika kukuza imani ya kiroho, kila mwanafunzi hufundishwa kumtegemea Mungu katika maisha yake ya kila siku, jambo linalosaidia kuunda viongozi waadilifu.
Kuhusu malengo ya muda mrefu, anasema ni kuhakikisha shule inakuwa miongoni mwa tatu bora kitaifa, na hatimaye ya kwanza ndani ya miaka 10.
Kupitia walimu wenye uwezo, mazingira bora na wanafunzi wenye nidhamu, lengo hili linaonekana kufikiwa.
Shule pia inalenga kuimarisha zaidi maabara za kompyuta na kuanzisha maktaba ya kidijitali ili kuendana na mabadiliko ya kidunia, pia kuwaunganisha wanafunzi na teknolojia ya karne ya 21.
Kwa kufanya hivyo, Joy inajenga daraja kati ya elimu ya kiasili na ile ya kidijitali.
Kwa kuweka mazingira salama na bora, Shule ya Joy imethibitisha kuwa watoto wa kike wanapopewa nafasi ya kusoma huonesha uwezo wao na kuondoa vikwazo vinavyoweza kuwakatisha tamaa.
Hii imeifanya shule kuwa ya kupigiwa mfano katika kukuza usawa wa kijinsia na kuwapa wasichana nafasi ya kufanikisha ndoto zao.
Sekondari ya Wasichana Joy si shule pekee, bali ni taasisi ya malezi, dira na matumaini kwa mtoto wa kike wa Tanzania na Afrika Mashariki.
Wazazi pia wamekuwa mabalozi wazuri wa shule, jambo ambalo uongozi unalithamini kwa dhati. Kwa mfano, mzazi Gloria Charles Kakwale, mama wa Precious Shadrack Madila (kidato cha tatu), amepewa zawadi maalumu ya ubalozi mzuri kama kielelezo cha ushirikiano kati ya shule na familia.
Kuhusu usajili wa wanafunzi, Septemba 23, 2025 shule itafanya usaili wa wanafunzi wa kidato cha kwanza kwa mwaka wa masomo 2026 jijini Dar es Salaam (Msimbazi Center) na shuleni Mbeya. Wazazi wanaohitaji kuandikisha watoto wao wanakaribishwa kushiriki.
Sekondari ya Wasichana Joy inabaki kuwa taa ya matumaini, chimbuko la viongozi wa baadaye na dira ya kuimarisha nafasi ya mtoto wa kike katika elimu na jamii.