Pemba. Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan ameahidi kuendelea kusimamia amani na utulivu, huku akiwataka Watanzania kujitokeza bila woga Oktoba 29, 2025 kupiga kura kumchagua Rais, wabunge na madiwani.
Amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita Serikali imejitahidi kusimamia utulivu wa kisiasa, usalama na amani ndani ya Tanzania, na hilo litaendelezwa wakati wote atakaokuwa madarakani.
Samia amesema hayo leo, Septemba 20, 2025, wakati akihitimisha ziara yake ya kampeni kisiwani Pemba, ambapo alifanya mkutano wa hadhara katika uwanja wa Gombani ya Kale, Wilaya ya Chake Chake, Kusini Pemba.
Mkutano huo wa kampeni ni wa tatu kwa mgombea huyo katika visiwa vya Zanzibar, kabla ya kuendelea na maeneo mengine ya Tanzania Bara.
“Miaka mitano yote hamjasikia chochote, labda mtu mwenyewe awe amejitokeza kwenda kuchokoza na kutaka kuvunja amani, ndiye atakayeshughulikiwa. Hata wale waliovuka mipaka na kutaka kuleta vurugu tuliwashughulikia, na hawajathubutu kurudi tena
“Kipindi hiki wengine wanakitumia kuchokozana, niwaombe msichokozeke. Kuweni kama mimi, nachokozwa sana lakini sichokozeki. Tusivunje amani kwa sababu ya uchaguzi. Sisi wote ni wamoja, sitafurahi kuona ndugu yangu kapigwa au kaumizwa, hivyo tutunze amani na utulivu,” amesema Samia na kuongeza:
“Msihofie kujitokeza kupiga kura….Tokeni, amshaneni, kapigeni kura, msiwe na hofu yoyote. Nafahamu bado kuna mengi, ila niwaahidi hakuna lisilozungumzika, lakini tusiende kuvunja amani kwa sababu eti kuna kitu hakijafanyika,” amesema.
Akinadi sera zake, Samia ameahidi kufungua milango ya biashara katika kisiwa cha Pemba kwa kuhakikisha uwanja wa ndege wa Pemba unajengwa kwa viwango vya kimataifa.
Amesema hatua hiyo itawezesha wageni na watalii wanaotaka kwenda Pemba kutua moja kwa moja kisiwani humo na kwamba hatua hiyo itawezesha pia kupungua kwa gharama za bidhaa katika kisiwa hicho, kwa kuwa mizigo kutoka mataifa mbalimbali haitalazimika kutua Unguja, kisha kusafirishwa kwa meli kwenda Pemba.
“Tukiujenga uwanja ule, ndiyo njia ya kufungua uchumi. Ndege kubwa zinazotoka Dubai, Muscat na kwingineko ziweze kutua hapa Pemba. Hata mizigo, sasa hivi tuna ndege za mizigo, tunataka mizigo inayotoka mataifa mbalimbali iende moja kwa moja Pemba,” amesema.
Amelitaja eneo lingine atakaloenda kushirikiana kikamilifu na mgombea urais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, kuwa ni ujenzi wa miundombinu katika kisiwa hicho ambayo ni ujenzi wa barabara ya Chake–Mkoani na bandari ya Wete.
“Barabara ya Chake–Wete inakwenda kukamilika, lakini kuna bandari kule Shumba inayotuunganisha na ndugu zetu wa Mombasa. Ikikamilika tutaachana na vimitumbwi, tutakwenda Mombasa kwa boti kubwa. Tunafungua usafiri wa watu na bidhaa na kwa ujumla milango ya biashara,” amesema.
Samia amesema katika kipindi cha miaka mitano Serikali yake na ile ya SMZ zimefanya mambo makubwa katikati ya mlipuko wa Uviko-19 uliosababisha kuyumba kwa uchumi wa dunia, na ana imani wanaweza kufanya makubwa zaidi katika kipindi kijacho.
Akizungumza katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Asha-Rose Migiro, amesema katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Samia ameimarisha umoja, mshikamano na kuitangaza Tanzania nje ya mipaka.
“Tuna uhakika akipata ridhaa tena atafanya makubwa zaidi ya haya. Taifa letu litasonga mbele na Pemba itasonga mbele. Nasimama hapa kumuombea kura za heshima na kishindo ili aendeleze kazi nzuri ambayo amekuwa akiifanya. Namuombea kura pia Dk Hussein Mwinyi ili kwa pamoja na Samia walipeleke mbele taifa letu,” amesema Dk Migiro.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah, amesema Samia ameendelea kusimamia umoja na mshikamano na mara zote amekuwa akihimiza mshikamano.
“Wale ambao wanaifahamu Pemba vizuri, zamani haikuwa hivi, lakini hii ni kwa sababu ya umoja, mshikamano na upendo wetu. Hii ni moja kati ya zile R nne alizoweka kama falsafa ya kuiongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Ombi langu, tuendelee kumtunza, kumheshimu, lakini pia kumchagua kwa kura za ndiyo, ili aendelee kuingoza nchi hii kwa miaka mitano ijayo,” amesema.
Mgombea ubunge wa Jimbo la Kojani, Hamad Chande, amesema ujenzi wa uwanja wa ndege Pemba na barabara ya Chakechake–Mkoani vitaenda kuchangamsha uchumi wa kisiwa hicho.
“Sisi wana Pemba tunakushukuru kwa mambo mengi uliyotufanyia. Umeweza kutafsiri ilani ya CCM kwa vitendo, kwa maana hiyo tunaahidi kukulipa wema kwa kukupigia kura. Hakuna mtu anayeweza kukalia kiti chako, wewe dereva wetu,” amesema Chande.
Mgombea ubunge Jimbo la Mkoani, Profesa Makame Mbarawa, amesema kwa kipindi alichosimamia sekta ya miundombinu na uchukuzi, ameshuhudia namna Samia alivyokuwa akihuzunishwa na miundombinu ya Pemba, ikiwemo uwanja wa ndege na barabara ya Chake–Mkoani yenye urefu wa kilomita 43.
“Uwanja wa ndege wa Pemba sasa unaenda kujengwa na kuwa wa kimataifa. Uwanja huu utakuwa na uwezo wa kuchukua abiria 300,000 hadi 700,000 kwa mwaka. Hii maana yake Pemba inaenda kufunguka kwenye sekta ya utalii na uchumi,” amesema.
Kwa upande wake mgombea ubunge wa viti maalumu Kaskazini Pemba (UWT), Asia Sharif Omary amesema Pemba imenufaika na miradi ya uwezeshaji inayogusa vikundi vya ushirika na wafanyabishara ndogondogo.
“Ilikuwa kero kubwa lakini kwa sasa mmeweza kuondosha kilio cha wananachi, ukweli ni kwamba watu wana matarajio makubwa na wewe kwa sababu umeanza vizuri na kuonesha nia kwa vitendo sasa hakuna mtu anayesubiri ajira ya Serikali.
“Hili ni matokeo ya uwekezaji mlioufanya kwa wajasiriamali, kwa namna ambavyo mmeyafikia makundi haya hatuna cha kufanya zaidi ya kuwalipa wema ifikapo Oktoba 29 wewe mama Samia na Dk Mwinyi,” amesema Asia.
Mgombea ubunge nafasi ya uwakilishi jimbo la Konde Kaskazini Pemba wilaya ya Micheweni Zawadi Amour Nassor amesema Samia alifanya jitihada kubwa kukabiliana na changamoto ya Uviko 19 aliyokutana nayo punde alipoingia madarakani.
“Changamoto hiyo ilimfanya aone haja ya kujenga hospitali katika wilaya ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya, kwa huduma tunazopata sasa usiwe na shaka wananchi wa Pemba watakuchagua ili nchi yetu izidi kung’ara,” amesema.