Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Jephte Kitambala wameiongoza Azam FC kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya El Merreikh Bentiu katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika iliyochezwa leo Septemba 20, 2025 kwenye Uwanja wa Taifa wa Juba, Sudan Kusini.
Katika mchezo huo ambao ulitawaliwa na Azam FC kwa muda mrefu, Fei Toto ndiye alianza kupachika bao la kwanza katika dakika ya 23 akimalizia mpira uliotemwa na kipa wa El Merreikh Bentiu baada ya krosi ya Pascal Msindo.
Bao hilo lilidumu hadi filimbi ya refa Dick Okello kutoka Uganda ilipopulizwa kuashiria muda wa mapumziko.
Azam iliongeza kasi ya mashambulizi katika kipindi cha pili na juhudi zake zikazaa matunda katika dakika ya 70 ilipopata bao la pili kupitia kwa Kitambala aliyeunganisha vyema pasi kutokea upande wa kushoto iliyopigwa na Baraket Hmidi.
Azam iliendelea kutawala mchezo na kuilazimisha Bentiu kujilinda katika dakika nyingi za kipindi cha pili lakini matokeo hayo hayakubadilika hadi filimbi ya mwisho ilipopulizwa.
Wawakilishi hao wa Tanzania sasa wanahitaji matokeo ya sare au ushindi wa aina yoyote katika nechi ya marudiano iotakayochezwa katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki ijayo ili wasonge mbele.
Katika raundi ya pili, mshindi baina ya Azam na El Merreikh Bentiu atakutana na mshindi kati ya KMKM na AS Port ya Djibouti.
Mambo hayakuwa mazuri kwa wawakilishi wa Zanzibar katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Mlandege baada ya kupokea kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Ethiopian Insurance katika mchezo uliofanyika jana kwenye Uwanja wa Abebe Bikila, Addis Ababa, Ethiopia.
Kichapo hicho kinailaizimisha Mlandege kupata ushindi wa tofauti ya mabao matatu au zaidi ili itinge katika raundi ya pili ya mashindano hayo na kinyume na hapo, itaaga mashindano au mshindi anaweza kupatikana kwa mikwaju ya penalti iwapo Mlandege itapata ushindi wa mabao 2-0.
Mshindi wa jumla baina ya Mlandege na Ethiopian Insurance atakutana na mshindi baina ya APR na Pyramids FC.