Dar es Salaam. Baada ya kifo cha Askofu mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dk Stephen Munga, Askofu Dk Benson Bagonza amesema walikuwa wamekubaliana kuzikana endapo mmoja wao angefariki dunia kabla ya mwenzake.
Dk Munga amefariki dunia alfajiri ya Jumamosi, Septemba 20, 2025, majira ya saa 9:30, akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rabinisia, jijini Dar es Salaam.
Marehemu Dk Munga alihudumu kama askofu wa dayosisi hiyo kuanzia mwaka 2001 hadi alipostaafu mwaka 2020.
Muda mfupi baada ya taarifa za kifo chake kutangazwa, Askofu wa KKKT Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza, ameeleza hisia zake kupitia ukurasa wake wa Facebook, akielezea ukaribu wake na marehemu.
Dk Bagonza aliandika kuwa baada ya kustaafu, Askofu Munga “alilazimika” kuishi na kutunzwa na Kanisa Anglikana, Dayosisi ya Tanga, linaloongozwa na Askofu Mkuu, Dk Maimbo Mndolwa.
“Kanisa Anglikana na kiongozi wake wanastahili tuzo isiyonyauka kwa wasamaria wema. Askofu Munga ameondoka, mimi nimebaki. Mtu akifa, mimi huwa nakabiliwa na changamoto nifanye nini?
“Nilie au nisilie/nikauke tu?! Kucheka siwezi na kulia siwezi. Kutamani kama ningekufa mimi, yeye akabaki. Kuhisi aliyekufa ananionea huruma mimi niliyebaki. Yeye anaenda mahali salama na mimi nimebaki katikati ya manyang’au,” amesema.
Amesema yeye na Askofu Munga walikutana Chuo Kikuu Makumira, akimtangulia darasa na yeye akiwa nyuma yake kabla hawajakutana Ulaya, Bagonza akiwa Chuo Kikuu Copenhagen na yeye na mkewe Aneth wakiwa Chuo Kikuu cha Lund.
Baadaye askofu alimtangulia mwaka mmoja katika nyumba ya maaskofu na waliposimama pamoja walishinda, walipotofautiana walishindwa kirahisi.
“Alikuwa kaka na mkewe dada/shemeji. Tangulia, siko mbali nawe. Wajaluo wana hekima isemayo, ‘Rafiki yako kufariki, bora afiwe ili umpe pole.’ Najiuliza, niende kumzika Askofu Munga? Rafiki yangu hawezi kuniona,” amesema.
Amesema yeye na Askofu Munga, Agosti 2023, waliwekeana ahadi ya kuzikana ikiwa mmoja kati yao atatangulia, huku akiweka bayana kuwa yupo tayari kumzika.
“Ameondoka kwanza, nitamzika. Sijui atakayenizika. Kama sitaliwa na mamba, waliobaki watanizika. Kama mimi ni mbaya, watanizika ili nisiwanukie. Kama mimi ni mzuri, watanizika ili kujiheshimu wenyewe. Pumzika Stephen. Ulikuwa faida kwa wengi kuliko tulivyokuwa hasara kwako,” aliandika.
Mbali na Dk Bagonza, alipozungumza na Mwananchi, Msaidizi wa Askofu huyo, Mchungaji James Mwinuka, amesema taarifa ya wapi atazikwa zitatolewa baada ya vikao, pale ndugu na jamaa zake watakapokutana kujadili.
“Tutawaeleza kama atazikwa nyumbani kwake Kijiji cha Maramba, Wilaya ya Mkinga, Tanga au kwingineko. Hii ni baada ya vikao, baada ya familia kukutana na kujadili,” amesema Mchungaji Mwinuka.
Hili limetokea wakati ambao siku mbili kabla ya kifo chake, Stephen Munga kupitia ukurasa wake wa Facebook aliandika ujumbe alioambatanisha na picha yake akiwa kitandani, akimshukuru Askofu Mkuu Maimbo Mndolwa wa Kanisa la Anglikana Tanzania na Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Tanga kwa kumpatia usafiri na wachungaji wa kumsindikiza Muhimbili kwa ajili ya kuhakiki afya yake.
“Namshukuru sana baba Askofu na wachungaji. Nilipata huduma nzuri sana kutoka kwa daktari wangu pamoja na wauguzi. Nashukuru sana daktari huyu aliyenihudumia kwa miaka mingi.
“Afya yangu iko vizuri kabisa, napambana na uzee tu unavyozidi kuongezeka. Nawashukuru sana mke wangu, wanangu, ndugu na jamaa. Mungu awabariki,” aliandika.