Manyara. Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kimeahidi kuja na fursa za ajira kwa vijana kwa kuanza na kilimo cha kisasa huku kikitengeneza mazingira bora ya upatikanaji wa viatilifu.
Katika hilo, chama kimeahidi kuja na maofisa ugani wa kutosha, kuwapa vijana maeneo yaliyohodhiwa, kupatikana kwa mbolea kirahisi ili walime, taifa liwe na chakula cha kutosha pamoja na biashara.
Hayo yamebainishwa leo, Septemba 20, 2025, katika Kata ya Daudi iliyopo Jimbo la Mbulu Mjini na mgombea mwenza wa urais kupitia Chaumma, Devota Minja.

Hizo ni miongoni mwa ahadi za Chaumma kupitia mikutano ya kampeni za urais, wabunge na madiwani zinazoendelea kuchanja mbuga kote nchini kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
“Tunataka tuondoe kodi kwenye matreta na mafuta ya petroli na dizeli ili watu wapate urahisi wa kusafirisha mizigo wao wenyewe na kulima kirahisi,” amesema.
Akizungumzia changamoto za ajira, amesema kuna vyuo zaidi ya 50 na kila mwaka wahitimu wapo lukuki wanakosa ajira, hivyo kikiingia madarakani, vijiana watapata ajira kikisema fursa ni nyingi hasa kwenye kilimo.
“Miaka 64 haiwezekani mkose lami, watu wa Mbulu ambao mnafanya kilimo. Nchi hii itaaunganishwa na lami wilaya kwa wilaya, mkoa kwa mkoa,” amesema.
Vitunguu vya Karatu vitauzwa duniani
Akieleza kuhusu zao la vitunguu linalolimwa Karatu alipokwenda kunadi sera, amesema Chaumma itahakikisha vitunguu hivyo vitatambulisha Tanzania kutokana na kuuzwa kwake kwa wingi nje ya nchi endapo Chaumma itapata ridhaa.

“Mbali ya kula, vitunguu vinatumika katika maeneo mengi ikiwemo utengenezaji wa dawa. Tutahakikisha kutakuwa na viwanda vya kutosha vya kuchakata kisha kuuza nje ya nchi,” amesema mgombea huyo.
Minja amesema Serikali ya Chaumma itahakikisha kitunguu kinakua zao kuu la biashara litakalonufaisha wakulima.
Mgombea ubunge wa Jimbo la Karatu, Fabiola Maami, amesema wakazi wa Karatu wanapaswa kuishi maisha mazuri kutokana na rasilimali walizobarikiwa ikiwemo ardhi ya kilimo.
“Wanalima vitunguu wananchi wa hapa, lakini wana umasikini. Hata nyumba wanazoishi zinaonesha. Barabara hazina lami, lazima tupate kiwanda cha vitunguu ili vichakatwe, vikauzwe hadi nje ya nchi,” amesema.
Amesema mbaazi, vitunguu na mazao yote lazima yalete maendeleo kwa wananchi kulingana na thamani yake.
Mgombea udiwani Kata ya Daudi, Paulo Sulle, amesema kero kubwa ya maji, huduma mbovu shuleni, kituo cha afya, na barabara inayowakabili itaenda kuisha wakipata madaraka.
“Kila kitongoji kitapata umeme, tutajenga zahanati za kutosha, maji, madaraja pamoja na ujenzi wa sekondari,” ameahidi.