Wadau wa mazingira wito jamii kupambana na taka za plastiki

Mwanza. Wakati dunia leo, Septemba 20, 2025  ikiadhimisha Siku ya Usafi Duniani, wadau wa mazingira wameitoa wito kwa jamii kuchukua hatua madhubuti dhidi ya utupaji holela wa taka, hususan za plastiki, ambazo zimeelezwa kuwa na athari kubwa kwa viumbe hai na mazingira kwa ujumla.

Akizungumza na wafanyabiashara wa soko la samaki Tampele baada ya kufanya usafi, Ofisa Mazingira wa Jiji la Mwanza, Fanuel Kasenene, amesema taka ngumu si tu zinaziba mifereji, mito na kusababisha mafuriko, bali pia zinatishia uhai wa viumbe pamoja na binadamu.

“Tunapotupa taka ovyo kwenye mitaro, mito na maziwa, tunajikuta tukikabiliwa na changamoto za mafuriko na mvua. Changamoto hizi zinatokana na utupaji mbaya wa taka. Taka zinapaswa kuhifadhiwa kwenye ngazi ya familia na kusafirishwa kwenye maeneo maalumu,” amesema Kasenene.

Baadhi ya wadau wa mazingira jijini Mwanza wakiandamana kuadhimisha siku ya usafi duniani. Picha na Saada Amir

Ameongeza kuwa takwimu zinaonesha mwaka 2024 dunia ilizalisha takriban bilioni 2.5 za taka, na kiasi hiki kikubwa cha taka, kinapokuwa hakikusanywi na kusafirishwa kwenye maeneo sahihi, huleta madhara makubwa.

“Duniani, takribani watu bilioni 2.7 hawana huduma za ukusanyaji taka, jambo linalosababisha madhara ya kiafya na kimazingira. Vilevile, viumbe hai vinakumbwa na tatizo hili… baadhi ya samaki wametoweka kutokana na wingi wa plastiki katika vyanzo vya maji,” ameeleza.

Akizungumzia Ziwa Victoria, Kasenene amesema, “Mwaka 2022 tulifanya tafiti katika mialo 69 ya Ziwa Victoria, na tukaona taka nyingi zikiwemo plastiki, nyavu na mabaki mengine. Lengo letu ni kuhamasisha wananchi kuhifadhi taka na kuzipeleka kwenye maeneo yaliyoidhinishwa.”

Baadhi ya vijana jijini Mwanza wakifanya usafi Mto Mirongo kuadhimisha siku ya usafi duniani. Picha Saada Amir

Akiwakilisha Shirika la Maendeleo na Ushirikiano wa Kimataifa la Ubelgiji (Enabel), Chris Laban amesema kutokana na kuona umuhimu wa usafi wa mazingira, shirika hilo limeanzisha mradi wa kulifanya Jiji la Mwanza kuwa safi na tanashati, unaolenga kuendeleza uchumi endelevu kwa kulinda mazingira, ukiwa na kaulimbiu ya ‘Ziwa letu, uchumi wetu.’

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Mamlaka za Serikali za Mitaa zinazozunguka Ukanda wa Ziwa Victoria (LVRLAC), Billy Brown, amewatahadharisha wananchi kudhibiti taka kwa kuunda umiliki wa pamoja na usimamizi bora wa taka ngumu, na kuwakumbusha umuhimu wa kulinda ziwa kama rasilimali muhimu ya Taifa.

Naye, Ofisa Afya Wilaya ya Nyamagana, Frolence Lugalabamu, amewataka wananchi kuzingatia kinga kwa kuwa ni bora kuliko tiba, na kinga ya magonjwa ya milipuko ni usafi.

“Kinga ni bora kuliko tiba. Usafi ni kinga muhimu dhidi ya magonjwa ya milipuko kama kipindupindu. Tunaweza kujikinga ikiwa tunahakikisha mazingira yetu yanabaki safi. Mwanza safi inawezekana,” amesema.

Ofisa Mazingira wa Shirika la Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo (EMEdo), Kitogo Lawrence, amesema takwimu zinaonesha takriban tani 600,000 za taka huzalishwa kila siku duniani, ambazo nyingi zikiwa ni plastiki zinazotajwa kuishi zaidi ya miaka 450.

“Taka hatarishi ni zile za plastiki. Chupa ya plastiki inaweza kuishi hadi miaka 450, hivyo kila mmoja anatakiwa kuchukua jukumu katika kupambana na taka za plastiki ambazo haziozi na zinaweza kuchangia mabadiliko ya tabianchi,” amesema.

Mkazi wa Mahina, jijini Mwanza, Mary Liberwa, amesema usafi unaanzia nyumbani, akiwataka wanawake kulinda mazingira kwa kutunza vizuri pampasi, akisema imekuwa moja ya kero katika mitaa mbalimbali ya jijini Mwanza.

“Usafi unaanzia nyumbani. Tunapaswa kuweka pampasi kwenye madampo badala ya kuachana nayo mitaani. Hii ni hatari kwa jamii,” ameeleza.

Siku ya Usafi Duniani ilizinduliwa Septemba 15, 2008, na lengo lake ni kuiepusha dunia na matatizo yanayosababishwa na uchafu, ikiwemo uchafu wa baharini.

Siku ya usafi huadhimishwa kwa watu kukusanya uchafu pamoja na kufagia, kazi ambazo hufanyika karibia kila mwaka kwa ajili ya utunzaji wa mazingira.