Mbeya. Mwili wa aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Mbeya, Shyrose Mabula, aliyeuawa kikatili kisha kuchomwa moto, umezikwa, huku waombolezaji wakipaza sauti kukemea tukio hilo, wakitaka wahusika wapatikane na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Maziko yamefanyika leo, Septemba 20, 2025, katika Makaburi ya Iwambi, mkoani Mbeya. Shyrose (21) alikutwa ameuawa, kisha mwili kuchomwa moto Septemba 16, zikiwa ni siku mbili baada ya baba yake mzazi, Dk Mabula Mahande, kuwasilisha taarifa kwa Jeshi la Polisi kuhusu kupotea kwa mwanaye Septemba 14.
Akizungumza wakati wa misa, Padri wa Kanisa Katoliki, Exavery Mwafimbo, amesema kila mmoja atakufa, lakini kifo cha Shyrose kimekuwa cha ukatili na mateso kuliko alivyostahili.

Amesema katika historia, alikuwa na haki na kwamba inaweza kutafsiriwa kuwa alikuwa bado anatafuta maisha.
“Mungu ilimpendeza kwamba mwanangu pumzika baada ya kuteseka na kuteswa na wakosaji, alikuwa bado anakomaa kiulimwengu,” amesema na kuongeza:
“Matukio ya maovu yameongezeka, lazima tukae kujadili, kujitafakari na kurejea somo la maadili, tumrudie Mungu. Jamii ifundishwe na kukumbushwa imani, watu hawasikilizi Mungu, wanasikiliza sauti zao binafsi.”
Ameshauri: “Turudi katika misingi ya utu, maadili na imani. Tuache ukatili wa namna yoyote, tenda kile unachoona hata wewe unastahili kutendewa na si vinginevyo.”

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Maryprisca Mahundi, akizungumza wakati wa kuaga mwili wa marehemu, amesema kila mmoja anapaswa kukemea na kulaani tukio hilo.
“Wamezima ndoto ya mtoto, baba na jamii kwa ujumla, hivyo waliohusika na tukio hilo wakapate stahiki yao,” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda, amesema Jeshi la Polisi lipo kazini kwa operesheni za usiku na mchana ili kuwakamata waliohusika na tukio hilo.
Amesema kila mmoja kwa nafasi yake ashiriki vyema kuwafichua wahalifu hao ili wakamatwe na sheria ichukue mkondo wake.
“Rais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu akikemea tukio hilo, akieleza si la Mbeya tu, bali hata kitaifa ni msiba mzito,” amesema Itunda, akitoa salamu za Serikali kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa.
Kwa niaba ya uongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Mbeya, Mshauri wa Wanafunzi, Frolence Kalimbikulu, amesema ni pigo kubwa kwa chuo hicho na Taifa kwa ujumla.

Amesema Shyrose alikuwa na matokeo mazuri katika masomo yake ya sheria.
“Chuo tumepoteza rasilimali kubwa na hata Taifa, alikuwa na matokeo mazuri na tumekuja nayo tunajiuliza, tutampa nani?” amesema.
Kiongozi wa mila, Chifu Rocket Mwashinga, amesema machifu watapiga magoti kumuomba Mungu ili waliohusika wakamatwe, ama kwa kujisalimisha au vyombo vya dola kuwatia nguvuni.
“Serikali ipo kazini, ama hao wahalifu wajitokeze kujisalimisha au wakamatwe, sisi machifu tutapiga magoti kumuomba Mungu wakamatwe wote,” amesema.
Shadrack Noel, mwanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe, amesema Shyrose alikuwa akishiriki shughuli za kijamii, ikiwamo kuwaona yatima, hivyo watatenga siku ya kumkumbuka na kuenzi kazi alizofanya enzi za uhai wake.
Lisa Siyame, akisoma wasifu wa Shyrose, amesema alizaliwa Desemba 25, 2004, jijini Mbeya, na katika uhai wake alipenda kujifunza.
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Mkoa wa Mbeya, Yassin Ngonyani, amesema Serikali ihakikishe hatua zinachukuliwa kwa waliohusika na tukio hilo, huku Katibu wa Siasa na Uenezi wa chama hicho, Mbeya Mjini, Philimon Mng’ong’o, akisema kutokana na ukubwa na uzito wa msiba huo, walilazimika kusimamisha shughuli za kampeni ili kutoa nafasi kwa makada kushiriki.