UKIWEKA kando kile kilichotokea usiku wa jana pale kwenye Dimba la Obed Itani Chilume lililopo Francistown, Botswana, Simba imewaandalia sapraizi mashabiki wake jijini Dar es Salaam ikiwa ni kuwafuta machozi baada ya kupigwa katika Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga.
Sapraizi hiyo ni katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali dhidi ya Gaborone United utakaochezwa Septemba 28, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na Simba inataka kuonyesha ukubwa wake na ubabe ikiwa nyumbani katika michuano ya CAF.
Usiku wa jana, Simba ilikuwa Botswana kukabiliana na Gaborone United na kabla ya mchezo huo, ilikuwa ikibebwa na rekodi bora dhidi ya timu za nchi hiyo kwenye michuano ya CAF.
Katika mara mbili ambazo Simba ilikwenda kucheza Botswana dhidi ya BDF XI mwaka 2003 na Jwaneng Galaxy mwaka 2021, ilishinda mechi zote za Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya mtoano, lakini mwaka 2023 ilitoka 0-0 dhidi ya Jwaneng Galaxy hatua ya makundi ya michuano hiyo.
Katika mechi za nyumbani dhidi ya timu hizo za Botswana, Simba iliichapa BDF XI, ikafungwa na Jwaneng Galaxy lakini mwaka 2024, ikalipa kisasi kwa Jwaneng ikiikanda mabao 6-0.
Kocha Mkuu wa Simba, FAdlu Davids, alisema: “Tumeifuatilia Gaborone United kwa kina, wapo imara na wagumu upande wa ulinzi, pia wapo vizuri katika kujipanga kushambulia. Ni mabingwa wa Botswana, hatuwezi kuwadharau.
“Kwenda hatua ya makundi unahitaji kushinda mechi zote za nyumbani na ugenini na sisi tumejiandaa kufanya hivyo.”
Kauli hiyo ya Fadlu inawapa matumaini mashabiki wa Simba wakirudi nyumbani, kuna kazi nyingine ya tofauti inakwenda kufanyika ya kuhakikisha timu inafikia malengo.
Simba katika michuano ya CAF inapocheza nyumbani, haijapoteza mechi 11 mfululizo, mara ya mwisho ilipoteza nyumbani Februari 18, 2023 ilipofungwa mabao 3-0 na Raja Casablanca katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Msimu huo Simba iliishia hatua ya robo fainali ikiondoshwa na Wydad Casablanca kwa penalti 4-3 baada ya matokeo ya jumla kuwa sare ya bao 1-1.
Baada ya kupoteza mchezo huo dhidi ya Raja, Simba ilishinda mechi tisa na sare moja kati ya 11 ilizocheza nyumbani. Mechi tisa zikipigwa Benjamin Mkapa, mbili zikichezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Matokeo ya mechi hizo yalikuwa hivi; Simba 1–0 Vipers, Simba 7–0 Horoya, Simba 1–0 Wydad, Simba 1–1 Power Dynamos, Simba 3–1 Al Ahli Tripoli, Simba 1–0 Bravos do Maquis, Simba 2–1 CS Sfaxien, Simba 2–0 CS Constantine, Simba 2–0 Al Masry, Simba 1–0 Stellenbosch na Simba 1–1 RS Berkane.
Kuna taarifa za Waarabu wa Morocco, Raja Casablanca kufikia makubaliano ya kuachana na aliyekuwa kocha wao, Lassaad Chabbi huku jina la Fadlu Davids likitajwa kuwa mbadala wake.
Taarifa kutoka Simba ni kuwepo kwa ofa hiyo imemfanya Fadlu kuwasilisha ombi la kuondoka.
Mtoa taarifa huyo alisema Fadlu ameomba mchezo wa jana dhidi ya Gaborone United uwe wa mwisho kwake, ili awahi anakotaka kwenda huku viongozi wa Simba wakimsubirisha kidogo wakimwomba abaki hadi mechi ya marudiano dhidi ya Gaborone United, kisha aondoke.
Katika Bodi ya Simba, mchakato wa siri sana umeshaanza kutafuta kocha mpya atakayekuja kuendelea alikoishia Fadlu.
“Tumemwomba atupe nafasi tujipange, unajua hii taarifa imekuja ghafla sana na mchakato wa kupata kocha siyo kitu rahisi hata kidogo, ni lazima mtulize akili.
“Bado hajatujibu lakini kwa kujiongeza tumeshaanza kujiandaa na maisha baada ya Fadlu, hatujajua anaweza kurudi na akasema nimeishia hapa.
“Bahati mbaya sana tupo katika mashindano, unaweza kuona presha anayotuachia sio rahisi tu kocha kukubali kuja haraka, anatakiwa afanye tathimini ya timu anayokwenda lakini na sisi kumjua ubora wake,” alisema bosi mmoja wa juu wa Simba.
Raja imeachana na Chabbi baada ya kuiongoza timu hiyo kwenye mechi mbili za ligi msimu huu akishinda moja na sare moja.
Kuondoka kwa kocha huyo, kunamfanya kuwa wa kwanza kuondolewa mapema zaidi akiwa hajapoteza mchezo hata mmoja katika Batola Pro.
“Ofa aliyowekewa kocha huyo ni mara mbili ya ile aliyopewa na Simba alivyokuwa anaongeza mkataba ambao ndio kwanza ameanza kuutumikia sasa.
“Suala la kocha kuvunja mkataba sio gumu kwani kunakuwa na vipengele vya makubaliano, naamini kutokana na presha iliyopo baada ya kupoteza dhidi ya Yanga sioni Fadlu akiendelea kubaki, ataondoka kwenda kujaribu changamoto nyingine nje ya Simba,” alisema mtoa taarifa huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.