Yaoundé. Brenda Biya, binti wa Rais wa Cameroon, Paul Biya, amewataka wananchi wa Cameroon kutompigia kura baba yake katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, akimlaumu kwa utawala usiofaa wa miaka 43 madarakani.
Paul Biya, ambaye ametawala Cameroon tangu mwaka 1982, ni miongoni mwa viongozi waliokaa madarakani kwa muda mrefu zaidi duniani.
Brenda, binti pekee wa Rais Biya, ameibuka hadharani na kuwaomba wananchi wa taifa hilo wasimpigie kura baba yake katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025.
Brenda, anayejulikana sana kwenye mitandao ya kijamii kwa jina la “King Nasty,” ametoa wito huo wakati wa matangazo ya moja kwa moja kwenye TikTok Live, ambapo alimtuhumu baba yake mwenye umri wa miaka 92 kwa kuingiza nchi kwenye umaskini, ukosefu wa ajira, na mkwamo wa maendeleo kwa miongo kadhaa.
Hii ni mara ya kwanza katika historia ya siasa barani Afrika kwa mtoto wa Rais aliye madarakani kumpinga waziwazi mzazi wake kisiasa.
Utawala wa Paul Biya umekuwa ukikabiliwa kwa muda mrefu na tuhuma za utawala wa kiimla, ufisadi mkubwa, ukiukwaji wa haki za binadamu, na chaguzi zenye utata.
Julai, Biya alitangaza nia yake ya kuwania muhula wa nane katika uchaguzi mkuu wa urais wa Oktoba 12, 2025. Taarifa hiyo ilitolewa kupitia akaunti yake rasmi ya X (zamani Twitter) kwa lugha ya Kifaransa na Kiingereza. Biya kwa sasa ndiye kiongozi wa taifa aliye madarakani mwenye umri mkubwa zaidi duniani.
“Mimi ni mgombea katika uchaguzi wa urais utakaofanyika Oktoba 12, 2025.
“Muelewe kuwa azma yangu ya kuwatumikia inalingana na changamoto kubwa zinazotukabili. Tukiwa pamoja, hakuna changamoto tutakazoshindwa. Bado mazuri zaidi yanakuja,” alisema.
Katika taarifa rasmi iliyopewa kichwa cha habari: “Tamko la kugombea uchaguzi wa urais Oktoba 12, 2025, kutoka kwa Mheshimiwa Paul Biya,” Rais huyo alisema:
“Kuhakikisha usalama na ustawi wa watoto wa nchi yetu pendwa na nzuri ni jukumu la heshima ambalo nimejitolea kwa moyo wangu wote tangu nilipochukua hatamu za uongozi. Hata hivyo, bado kuna mengi ya kufanywa. Katika mazingira ya kimataifa yanayozidi kuwa magumu, changamoto tunazokabiliana nazo zinazidi kuwa za dharura. Katika hali hii, siwezi kujiondoa kwenye jukumu langu.”
“Nimeamua kuitikia wito wa mara kwa mara kutoka katika mikoa yote kumi ya nchi yetu pamoja na waishio ughaibuni. Bado mazuri zaidi yanakuja,” alisisitiza tena.
Katika video hiyo, ambayo Brenda (27) aliirekodi akiwa nchini Uswisi, alisema kwamba atakatisha mawasiliano kabisa na wazazi wake na kudai kuwa familia yake imemtendea vibaya, huku akiongeza kuwa watu wa karibu naye wanamtakia kifo.
Baadaye aligeukia masuala ya kisiasa na kusema wazi kwamba hatampigia kura Paul Biya, na kwamba anatumaini Cameroon itapata rais mwingine.
Video hiyo imesambaa sana mitandaoni (imekuwa viral) na kupokelewa kwa mikono miwili na upinzani wa kisiasa nchini Cameroon. Hadi sasa, hakuna tamko lolote rasmi lililotolewa kutoka Ikulu au serikalini.
Imeandikwa na Noor Shija kwa msaada wa mtandao